MAISHA bila ya unafiki huwa hayaendi. Kwa haraka haraka nilikuwa nikikifuatilia kikosi cha Taifa Stars kilichotajwa katika dakika za mwisho na kocha wake, Adel Amrouche ambacho jana kilitarajiwa kucheza dhidi ya Sudan pale Saudia Arabia pambano la kirafiki.
Nilikuja kugundua maisha bila ya unafiki huwa hayaendi.
Unafiki wa kwanza ambao umesababisha tupige kimya kuhusu uteuzi wa kikosi hicho ni ukweli Taifa Stars yenyewe imefuzu fainali za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) zitakazofanyika mwakani pale Ivory Coast.
Kama ingekuwa haijafuzu basi Kocha Amrouche angekutana na maneno makali yanayohusu uteuzi wa kikosi chake kwenye pambano la kirafiki dhidi ya Sudan.
Kwa sababu Stars ilirudi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikiwa imefuzu kwenda Afcon ikitokea Algeria basi mambo mengi yamefunikwa na watu wameacha kombe lifunikwe ili mwanaharamu apite.
Ingekuwa vinginevyo basi kuna mambo mengi ambayo yangejadiliwa.
Kitu cha kwanza kabisa ni namna watu hawakujadili tena kuwepo au kutokuwepo kwa mabeki wa pembeni wa Simba, Mohammed Hussein Tshabalala na Shomari Kapombe.
Hawajaitwa katika hiki kikosi na hakuna ambaye ameshangaa. Kuanzia mashabiki, viongozi wa klabu zao hadi waandishi na wachambuzi hakuna aliyeshangaa.
Unajua kwa nini? Sababu ni mbili. Kwanza kabisa ziliwahi kupigwa kelele wakati pambano la Stars dhidi ya Uganda pale Ismailia likikaribia.
Hawa rafiki zetu waliachwa halafu Stars ikashinda dhidi ya Uganda. Pambano la marudiano rafiki zetu waliitwa halafu tukafungwa pale Temeke. Ilikanganya watu kidogo.
Lakini kwa upande ule anaocheza Tshabalala alipangwa Novatus Dismas ambaye kiwango chake kilikuwa cha hali ya juu. Tangu wakati huo hadi sasa Novatus amekuwa katika kiwango cha hali ya juu huku akionyesha umahiri mkubwa na uzoefu anaoendelea kujikusanyia katika soka la Ulaya. Tumekuwa wanafiki baada ya kuona hakuna kinachoharibika.
Halafu mwanzo wa msimu huu kulizuka kelele Kapombe na Tshabalala wamechoka. Ni baada ya Simba kuanza kwa mwendo wa kusuasua katika msimu wake. Mara nyingi wachezaji wetu mahiri wanapoachwa katika kikosi cha timu ya taifa basi kelele nyingi za malalamiko huwa zinavuma kutoka kwa mashabiki wao.
Kuna Usimba na Uyanga mwingi katika suala la timu ya taifa.
Hakujakuwa na kelele kwa sababu dunia ingewashangaa watu wale wale waliokuwa wanalalamika kuchoka kwa Kapombe na Tshabalala ndio watu wale wale ambao wangekuwa wanalalamikia kuachwa kwa wachezaji hao katika kikosi cha timu ya taifa. Haishangazi kuona watu wameamua kupiga kimya tu.
Kama kusingekuja na hoja ya malalamiko kuhusu suala la kuchoka kwao leo mashabiki lukuki wangeibuka na hoja ya kwa nini nafasi ya Kapombe imekwenda kwa Israel Mwenda ambaye anapigwa benchi na Kapombe kikosi cha Simba.
Tumeamua kupiga kimya kuhusu hilo jambo kwa sababu tayari tulishasema Kapombe kachoka.
Halafu kuna suala la Fei Toto. Kuna rafiki zangu wamekaa kimya baada ya Fei Toto kuachwa katika kikosi cha Taifa Stars. Kisa? Ameondoka katika klabu zao.
Fei, bora kama alivyo, kama angekuwa katika timu kubwa za Kariakoo basi tungesikia malalamiko mengi kuhusu kuachwa kwake.
Msimu huu katika ligi ameshafunga mabao matatu. Haijalishi kama alifunga katika pambano dhidi ya Tabora United iliyokuwa na wachezaji nane uwanjani katika pambano dhidi ya Azam pale Mbagala.
Kama yale mabao Fei angefunga akiwa na Yanga au Simba basi yangekuwa kitu kikubwa katika soka letu.
Kocha wa Stars angekuwa na presha kubwa ya kumjumuisha Fei katika kikosi cha Stars kama angekuwa mchezaji wa Yanga. Na baada ya mabao yale angekuwa katika presha zaidi. Hata hivyo, hajakuwa katika presha kwa sababu anacheza Azam. Huu unaitwa unafiki.
Lakini nadhani wanaona namna wanaume fulani wanavyopiga kazi katika eneo la kiungo cha Stars.
Kuna Mzamiru Yassin, Sospeter Bajana na Mudathir Yahya pamoja na Himid Mao wamekuwa wakipiga kazi ya kutosha katika eneo la kiungo. Hawa kwa namna moja au nyingine walistahili sifa kubwa kuliko kumkumbuka Fei.
Kitu kingine ambacho kimejificha katika unafiki wetu kuhusu Stars ni ukweli kocha Amrouche ameita wachezaji 12 wanaocheza soka nje ya nchi. Mara ngapi tumekuwa tukiimba kuhusu umuhimu wa wachezaji wanaocheza nje katika kikosi cha Stars?
Mara ngapi tumekuwa tukisisitiza kuhusu umuhimu wa kuwa na wachezaji wengi wanaocheza nje katika kikosi cha Stars?
Tunaamini wachezaji hawa huwa wanakuwa na kitu cha ziada zaidi kwa sababu wacheza katika ligi ambazo zina ushindani zaidi kuliko Ligi yetu. Hii ni hatua kubwa kwa soka letu.
Kwa nini hatushangilii hatua hii? Kuna zile nyakati ambazo tulikuwa tunasema ‘Laiti kama tungekuwa na wachezaji 10 wanaotoka nje basi Stars ingefika mbali’. Leo mbona tunakaa kimya? Nadhani kwa sababu bado hisia zetu zipo kwa wachezaji wa Simba na Yanga. Hawa ndio ambao wanatengeneza mijadala wakati wa uteuzi. Ni kama ambavyo Tshabalala na Kapombe walitutengenezea wakati ule.
Nini kinafuata? Tukiachana na unafiki wetu wa hapa na pale naona kwa sasa tuna wachezaji ambao wanaweza kusababisha walau tucheze mpira unaoeleweka kulinganisha na kile kikosi cha Stars kilichocheza katika michuano ya Afcon 2019 pale Misri.
Walau sasa hivi tunaweza kupiga pasi kadhaa kulinganisha na kikosi cha Emmanuel Amunike.
Kundi letu ni gumu. Dhidi ya Morocco na majirani zetu Zambia na DR Congo maisha yatakuwa magumu lakini mpira utapigwa.
Kitu cha msingi zaidi ni Watanzania wajiandae kufurahia kuwepo katika michuano hii kuliko kutupa lawama nyingi kama timu haifanyi vizuri. Tunajenga tena timu mpya ambayo ina wachezaji wengi wapambanaji.
Kuna makundi mawili. Kundi la wachezaji wanaocheza nje na kundi la baadhi ya wachezaji wa ndani ambao klabu zao zimekuwa zikifanya vyema katika michuano ya CAF.
Wachezaji wa Simba na Yanga wanatusaidia katika hilo hata kama baadhi wameachwa.