Dar es Salaam. Kesi ya unyang'anyi wa kutumia nguvu inayowakabili watu watatu, akiwemo Koplo wa Polisi, itaanza kuunguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuanzia Oktoba 12, 2023, ambapo upande wa mashtaka utawasomea hoja za awali (PH), washtakiwa hao.
Askari Polisi huyo mwenye namba F 5867 Koplo Khamisi (40), pamoja na wenzake, wanakabiliwa na shtaka moja la unyang'anyi wa kutumia nguvu na kujipatia Sh78.6 milioni.
Uamuzi huo umetolewa leo Oktoba 5, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Amir Msumi wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa hoja za awali.
“Kutokana na upelelezi kukamilika na upande wa mashtaka mnaomba kupewe siku chache ili muweze kukamilisha hoja hizo za awali, hivyo naahirisha kesi hii hadi Oktoba 12, 2023 kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo yao," amesema Hakimu Msumi.
Awali, Wakili wa Serikali Judith Kyamba, alidai kuwa shauri hilo lilitwa mahakamani hapo kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa hoja za awali, lakini upande wa mashtaka bado hawajakamisha kuandaa hoja hizo.
“Mheshimiwa hakimu kutokana na hali hii, tunaomba mahakaka itupe siku chache ili tuweze kukamilisha na kuja kuwasomewa hoja za awali washtakiwa hawa," alidai Wakili Kyamba.
Hakimu Msumi baada ya kusikiliza maelezo hayo, alihirisha kesi hiyo hadi Oktoba 12, 2023.
Mbali na Koplo Hamisi, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 173/2023 ni pamoja na dereva Nassoro Mkono (32) maarufu kama Samson na mkazi wa Mbezi Kimara, pamoja na Sia Tarimo (26) mkazi wa Ukonga.
Katika kesi msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa Mei Mosi, 2022 huko Ukonga, eneo la Karakata Aiport, lililopo Wilaya ya Ilala.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kufanya unyang'anyi wa kutumia silaha na kujipatia Sh78.6 milioni, mali ya Zawia Shabani.
Na kabla ya kujipatia fedha hizo, washtakiwa hao walitumia nguvu na kumtishia ili waweze kujipatia fedha hizo bila kikwazo.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Septemba 21, 2023 na kusomewa