KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi alikuwa jukwaani akiwasoma wapinzani wao kwenye Ligi Kuu Bara, Simba ambao watakutana nao mwezi ujao, lakini pia Al Ahly ambao wapo nao kundi moja kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, kisha akaficha mafaili yake kiakili.
Gamondi alikuwa jukwaani kwenye mchezo huo wa juzi kati ya Simba dhidi ya Al Ahly uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 akiwa sambamba na meneja wa Yanga, Walter Harrison wakionekana kuwa bize na mchezo huo huku wakionyeshana vitu mbalimbali na kuandika kila mara.
Mara baada ya mchezo huo kumalizika Gamondi hakutaka kufunguka kwa undani kueleza ubora wa timu zote mbili akisema alikwenda uwanjani kuangalia mechi pekee na siyo kuwasoma wapinzani wake.
Kocha huyo alisema akili yake kwa sasa ipo kuwatazama wapinzani wao kwenye Ligi Kuu Bara, Azam FC watakaokutana nao kesho kwenye uwanja huo na wala hakwenda kuangalia au kuwasoma Simba ama Ahly.
“Nimekuja kuangalia mechi hii hakuna kingine. Niliona tuna nafasi nikaamua kuja na meneja wangu. Sisi ni timu ya soka siyo suala geni kuwa hapa,” alisema Gamondi huku akitabasamu kuonyesha kuwa ana jambo.
“Nimefurahi kuona mechi nzuri kila timu ilicheza vizuri kipindi kimoja. Hakuna kingine ninachoweza kuongeza kwa sasa unajua kwamba akili yangu na wachezaji wangu ni mchezo wa Jumatatu dhidi ya Azam usisahau ni mechi ngumu ile.
“Tunahitaji muda wa kuangalia sana kuhusu Azam kuliko jambo lolote. Tutakwenda kukutana na moja ya timu bora kwenye ligi lazima tuwaheshimu.”
Yanga itakuwa uwanjani kesho kuvaana na Azam, ukiwa ni mtihani mwingine kwa kocha huyo ambaye ameshapoteza mchezo mmoja wa ligi hiyo hadi sasa dhidi ya Ihefu SC.