Bariadi. Nshola Kabadi, mama mzazi wa watoto mapacha waliofariki dunia kwa madai ya kupakwa dawa na mganga wa kienyeji kuoteshwa matiti ili waweze kuolewa ameendelea kusota mahabusu ya polisi kwa zaidi ya siku saba.
Nshola, mkazi wa kijiji cha Nkololo Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu anashikiliwa na polisi tangu Oktoba 4, mwaka huu kwa mahojiano kuhusiana na vifo vya watoto wake, Pendo Saku na Furaha Saku (17) waliofikwa na mauti baada ya kupelekwa kwa mganga kupakwa dawa ya kuotesha matiti ili waolewe.
Inadaiwa mama wa mapacha hao waliohitimu kidato cha nne mwaka 2022 alifikia uamuzi huo baada ya binti zao kuchelewa kuota matiti.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, baba mdogo wa mapacha hao, Meli Saku alisema shemeji yake hajaachiwa tangu Oktoba 4, mwaka huu alipokamatwa na polisi.
Ingawa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe ameahidi kutoa taarifa za tukio hilo baadaye, uthibitisho kutoka kwa familia umethibitisha kuwa mama huyo anaendelea kushikiliwa.
Mapacha hao tayari wamezikwa katika Kijiji cha Nkololo Wilaya ya Bariadi.
Msako dhidi ya mganga
Ofisa wa Mawasiliano kwa Umma wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Mohammed Sakoty aliyezungumza kwa niaba ya Kamanda Swebe amesema msako unaendelea kumafuta mganga wa kienyeji anayedaiwa kuwapaka dawa watoto hao ambaye alitoroka mara baada ya tukio.
"Mganga anayetuhmiwa kuhusika na vifo hivyo bado hajakamatwa na tunaendelea kumsaka. Tutawajulisha mtuhumiwa hiyu akikamatwa," ilisema Mohammed kwa niaba ya Kamanda Swebe