HUKU wakitarajiwa kuvaana na Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa leo Alhamisi kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amechimba mkwara mzito kwamba, kurejea kwa wachezaji wao wawili, Aishi Manula na Luis Miquissone kutarejesha moto wa kikosi chao.
Manula ambaye alifanyiwa upasuaji wa nyonga mwezi Juni mwaka huu, alikosa sehemu kubwa ya mechi za Simba za mwishoni mwa msimu uliopita, ambapo juzi Jumanne alianza rasmi programu za mazoezi ya pamoja na timu, kwa upande wa Miquissone yeye aliukosa mchezo wa marejeano dhidi ya Power Dynamos kutokana na kukosa utimamu wa mwili.
Akizungumza na Spoti Xtra, Ally alisema: “Kama kuna taarifa ambayo mashabiki wengi wa Simba walikuwa wanaisubiri kwa hamu ni suala la kurejea kwa Aishi Manula kutokana na kukosekana kikosini muda mrefu, kuanza kwake mazoezi kunamaanisha sasa lango letu litazidi kuwa imara na kutakuwa na ushindani mkubwa wa namba.
“Lakini Luis ambaye pia tulimkosa kwenye mchezo dhidi ya Power Dynamos amerejea na kusafiri na timu kwa ajili ya mchezo huu, tunaamini mjumuiko huu utazidi kuongeza makali ya kikosi chetu na kuturejesha kwenye ubora.”
STORI NA JOEL THOMAS