NI mechi 21 Sasa tangu Kocha Robertinho aanze jukumu la kukiongoza Kikosi cha Simba SC. Hajapoteza mchezo wowote ndani ya dakika 90.
Ni Mbabe kweli kweli. Anastahili heshima japo kuna muda anatudanganya. Kuna namna Kocha Robertinho anatuchukulia poa. Mpira wa miguu pamoja na kuheshimu taaluma, bado unabakiwa kuwa mchezo wa wazi.
Bado unabaki kuwa ni mchezo wa maoni. Nahodha wa Simba, John Raphael Bocco ndiyo mchezaji mzawa aliyefunga mabao mengi ya ligi yetu kuliko yoyote katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.
Hakuna Shaka atabaki kuwa moja ya washambuliaji bora tuliowahi kuzalisha nchini. Kila nikimtazama siku hizi, nafsi yangu inaniambia tayari amemaliza. Mwili umeanza kukataa. Nayaona mapumziko yake kisoka kama shujaa wetu hayako mbali.
Robertinho hataki kukubaliana na ukweli kuwa, Bocco yuko maji ya jioni. Kwa ukubwa wake na rekodi zake, bado anaweza kuchangia kitu lakini sio kwenye kila mechi.
Mechi ngumu Kama dhidi ya Yanga, Azam, Wydad Casablanca na Al Ahly, kumtegemea Bocco ni kutudanganya. Sisemi asicheze. Sisemi hawezi kuamua mechi. Ninachosema, muda wake wa kuwa tegemeo umeondoka. Kuendelea kutaka Bocco awe kijana ni kutudanganya. Labda TV yangu iwe inanidanganya.
Labda macho yangu hayaoni vizuri siku hizi. Hebu nipe maoni yako juu ya uwezo wa Bocco wa Sasa pale Simba. Labda Mimi nina Gubu. Labda mimi sitazami vizuri. Niandikie ujumbe wako wa maandishi kupitia namba yangu ya Simu hapo chini.
Pale Yanga wanashida ya mshambuliaji lakini Clement Mzize wanayemlalamikia, ni bora kuliko mshambuliaji mwingine yoyote pale. Ni rahisi sana kukuelewa Kocha Gamondi. Hamna namna.
Licha ya mapungufu ya Yanga, lakini Mzize ndiye mshambuliaji wao bora aliyepo. Pale Simba, naona Kocha Robertinho anatudanganya. Sio kweli kwamba hakuna mshambuliaji bora kuliko Bocco.
Moses Phiri na Jean Baleke kwa zama hizi ni bora sana zaidi ya Bocco. Kumuanzia Bocco kwenye mechi dume huku benchi ukiwa na Phiri na Baleke ni kutudanganya. Ni uongo wa wazi wazi.
Bocco hawezi kurudi ujana. Nina heshima kubwa sana kwa Bocco. Amefunga sana mabao lakini hata kila Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, leo hawako Ulaya tena. Nyimbo za Klabu Bingwa Ulaya zinapigwa leo bila wao kuwepo. Sio kwamba Messi amekwisha kabisa.
Sio kwamba Ronaldo amekwisha kabisa. Muda wao umekwisha. Zama zao zimemalizika. Tutabaki tu kuwaheshimu lakini hatuwezi kuwategemea tena.
Mimi sio Kocha lakini mchezo wa soka ni mchezo wa wazi. Mchezo wa Soka ni mchezo wa maoni. Kocha Robertinho aache kutudanganya. Historia na rekodi za Bocco zitabaki kama wimbo usioisha utamu lakini kumfanya kuwa mshambuliaji chaguo la kwanza ni uongo. Ni kutudanganya mchana kweupe. Labda kama macho yangu hayaoni vizuri siku hizi.
Labda kama TV yangu inanidanganya. Bado anaweza kuisaidia timu lakini asitumike kama tegemeo la timu. Wewe unamuonaje Bocco? Niandikie ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo chini.
Mchezaji siku zote anaongezeka uwezo wa kucheza. Hakuna benchi linaloweza kukutengenezea mchezaji bora. Nadhani ni muda sasa wa kuanza kuwatumia Phiri na Baleke.
Mechi ya kufuzu Klabu Bingwa Afrika ugenini dhidi ya Power Dynamos ilisubiri mpaka Baleke aingie kipindi cha Pili ndiyo ichangamke. Mechi ya juzi pale Cairo, ilisubiri mpaka Baleke aingie ndiyo ichangamke. Hapo nimetaja kwa ufupi tu. Hapo nimetaja kidogo tu. Robertinho aache kutudanganya.
Pale Simba washambuliaji wapo. Tatizo ni yeye tu na uteuzi wake wa kikosi cha kwanza. Bocco bado anahitajika lakini sio tegemeo tena. Ukubwa wake na rekodi zake ziheshimiwe lakini Phiri na Baleke waaminiwe na Kocha. Najua una maoni pia tofauti kwa sababu mpira ni mchezo wa wazi.
Najua una maoni tofauti kwa sababu soka ni mchezo wa maoni. Kama una lolote usisite kuniandikia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya Simu hapo chini. Robertinho aache kutudanganya. Kasi ya Bocco imepungua. Ufanisi wale mbele ya lango umepungua pia. Apewe maua yake lakini asiwe tegemeo la timu kwa sababu kwa sasa anaelekea ukingoni. Nguvu za Mwanadamu ni kitu cha kuisha. Hata Mimi na Wewe kuna muda nguvu zetu zitapungua. Kuna siku zitaisha. Hatutaweza tena kwenda Uwanjani.
Hatutaweza tena kusafiri kwenda kuangalia mechi mikoani. Ni suala la muda tu. Mosses Phiri na Jean Baleke wapewe nafasi. Wajengewe Hali ya kuaminiwa kuna watu watakiongeza kwenye kikosi cha Mnyama.
Pamoja na rekodi nzuri sana aliyonayo Kocha Robertinho tangu ajiunge na Simba, Mashabiki na Viongozi wanamdai taji. Bila kuwapa Kombe kubwa lolote msimu huu, watu watasahau kila kitu kuhusiana na rekodi zake.
Rekodi bila taji ni namba tu kama namba nyingine. Robertinho ni lazima abadilishe gia angani. Mpira wa Miguu ni mchezo wa magoli. Mpira wa miguu ni mchezo wa kukimbia. Wanahitaji watu wa kufunga Magoli pale mbele. Wanahitajika watu wa kukimbia kila wakati kila mahali. Mchezaji kama Bocco hawezi kukupa vitu hivyo mfululizo.
Leo anaweza kukupa, atakupa tena baada ya mechi Tano. Ni muda wa Baleke na Phiri kuaminiwa na kujengwa kisaikolojia. Tunampenda sana Bocco lakini hawezi tena kufunga kama zamani. Tunamuheshimu sana Bocco lakini hawezi tena kukimbizana uwanjani kila siku.
Ni mchezaji wa matumizi maalumu. Ni mchezaji wa baadhi ya mechi. Anahitaji matumizi sahihi uwanjani tofauti na zamani. Kama una maoni yoyote, nimekaa palee nasubiri ujumbe wako wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo chini.