Pambano linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini la Yanga dhidi ya Azam FC lililopangwa kufanyika Jumatano ya Oktoba 25, sasa litapigwa Oktoba 22, baada ya Bodi ya Ligi (TPLB) kufanya mabadiliko ya mechi za raundi ya sita ya Ligi Kuu.
Timu hizo zinafukuzana katika msimamo, Azam ikiwa ya pili, huku Yanga ikifuatia nyuma baada ya kila moja kucheza mechi tano na kwa siku za karibuni zimekuwa na upinzani mkali na kwa msimu huu zimeshakutana kwenye Ngao ya Jamii na Yanga kushinda 2-0, wakati kwa msimu uliopita Yanga ilishinda mechi ya marudiano kwa 3-2 wakati ile ya awali ilikiisha 2-2.
Rekodi zinaonyesha Azam iliifunga Yanga mara ya mwisho Aprili 25, 2021 kwa bao la Prince Dube na mechi tano zilizofuata imeambua sare moja tu na kupoteza nne ikiwamo ya Ngao ya Jamii Agosti 9, jijini Tanga, hivyo mechi hiyo ya kwanza ya ligi kwa msimu huu itakuwa ya kulipa kisasi.
Mabadiliko ya ratiba yaliyotangazwa jana na TPLB, imefafanua sababu ya kufanya hivyo ni kutolewa kwa timu za Azam FC na Singida Big Stars kimataifa, lakini pia ushiriki wa Simba kwenye African Football League na kutokuwepo kwa mechi za mchujo za Chan 2024.