Tukio la kugundulika kwa mwili wa marehemu limetokea mapema jana Ijumaa Oktoba 13, 2023 baada ya waosha magari kusikia harufu kali iliyokuwa ikitoka ndani ya gari hilo.
Eneo hilo ambalo limegeuzwa maegesho ya magari baada ya Jiji kuzivunja nyumba zake, limekuwa ni maarufu kutokana na kutumiwa na madalali kuuza magari na kuoshwa magari.
Askari Polisi walifika eneo la tukio na kuukuta mwili huo uliokuwa kwenye gari dogo aina ya Scudo iliyokuwa imeegeshwa eneo hilo kwa zaidi ya siku tatu.
Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha, Justine Masejo amethibitisha kutokea tukio hilo huku akisema uchunguzi umeanza.
Baadhi ya mashuhuda walidai kuwa marehemu Mallya amekuwa na tabia ya kufika eneo hilo na kuegesha gari lake na kisha kwenda bar iliyopo eneo hilo kwa ajali ya kula chakula na kunywa.
Mwenyekiti wa eneo hilo maarufu kwa wauzaji wa magari (madalali), Alex Kahela amesema alipata taarifa asubuhi ya leo oktoba 13, kuhusiana na tukio hilo na baada ya kufika aliweza kulitambua gari hilo kuwa ni mali ya mfanyabiashara huyo.
"Baada ya kupata taarifa nilifika eneo la tukio na kujaribu kuchungulia ndani ya gari hiyo lililokuwa limefungwa milango kwa ndani tukiwa na watu wengine tuligundua kuwa mwili uliopo ndani ni wa mzee Mallya," amesema.
Amesema hafahamu chanzo cha kifo chake na mwili huo wanakadiria kuwa ndani ya gari hilo kwa siku mbili au tatu bila kughundulika hadi leo harufu iliyokuwa ikitoka katika gari hilo iliwashtua watu hao.
Muosha magari Juma Jumapili alisema jana jioni walianza kusikia harufu hiyo hata hivyo haikuwa kali sana na kujikuta wakiendelea na shughuli zao ila leo kwa sababu kumekucha na jua kali harufu iliongezeka na kuwa kali zaidi.
Shuhuda mwingine Peter Kivuyo amesema kuwa baada ya kusikia harufu kali walisogelea gari hilo na walipochungulia ndani ndipo walipogundua kuna mwili wa mtu akiwa haongei.
Amesema alipoutazama vizuri mwili huo aliweza kumtambua kuwa ni Mzee Mallya huku pembeni ya mwili kukiwa na mabunda ya fedha na waliona michirizi ya damu eneo la kifua.
"Niliuona mwili wa marehemu sehemu ya kifua kukiwa na michirizi ya damu huku pembeni akionekana ameshika fedha," amesema.
Ismail Juma akizungumzia tukio hilo alitaka Jiji la Arusha kulisimamia eneo hilo kwani kunaweza kutokewa matukio ya hatariii zaidi.
"Jiji walivunja nyumba hapa na sasa eneo limegeuzwa bar, sehemu ya kuosha magari na kuuza magari," amesema.