Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru mshtakiwa Frida Nzogaya baada ya upande wa mashtaka kishindwa kuthibitisha shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu 323.52.
Hukumu hiyo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio amesema upande wa mashtaka ulileta mashahidi watano ambao hata hivyo ushahidi wao haukutosha kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo.
Mrio amesema kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo kwa kuwa umeacha shaka kulingana na namna tukio lilivyotokea.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka inadaiwa kuwa Agosti 15, 2019 katika ofisi za Posta mkoani Dar es Salaam, Frida alikutwa akisafirisha chupa 12 za bangi zenye uzito wa gramu 323.52.
"Kwa kuwa chupa 12 hazikuweza kuonesha ni kitu gani ambacho kilikuwa ndani hivyo isingekuwa rahisi kwa mshtakiwa kujua kama aliletewa mzigo tofauti," amesema Shaidi.
Katika utetezi wake mshtakiwa huyo amedai kuwa aliagiza mzigo kupitia njia ya mtandao, mzigo ambao ulikuwa dawa ya saratani na alipofika katika ofisi za posta alipewa namba ya malipo kisha akafanya malipo kwa ajili ya kuchukua mzigo wake ndipo alipokamatwa na kuelezwa kuwa zilikuwa ni dawa za kulevya.
Pia jambo lingine ambalo liliacha shaka katika kesi hiyo ni namna ambavyo mshtakiwa hakukabidhiwa mzigo huo baada ya kufanya malipo, badala yake maofisa walibaki nao na kumwambia kuwa ni bangi.
Mrio alisema kutokana na hayo mahakama hii inamuachia huru mshtakiwa huyo.