Winga wa Power Dynamo Joshua Mutale amefunguka kuhusu mahaba yake na Klabu ya Yanga ya Tanzania baada ya kuonekana akiwa amevalia jezi ya Wananchi huku picha yake hiyo ikisambaa vilivyo kwenye mitandao ya kijamii.
Licha ya kutolewa na Simba Sc kwenye michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika, Mutale ameonyesha uwezo mkubwa kwenye michezo yote miwili nyumbani na ugenini jambo lililowaibua vigogo wa Simba na kuanza harakati za kunyatia saini yake kwenye dirisha dogo la usajili.
Mutale ni winga wa boli ana uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira na kupiga chenga, uwezo wa kuvunja mstari wa mwisho wa mabeki, kupiga pasi za mwisho, amefanya hivyo kwenye mechi tatu alizocheza na Simba kuanzia Simba Day.
Joshua amesema ana urafiki wa Karibu na Mchezaji wa Yanga, Kennedy Musonda ambaye pia ni raia wa Zambia na jezi ambayo picha yake ilisambaa akiwa amevaa alipewa kama zawadi na Musonda.
“Baada ya mechi dhidi ya Simba nikaona mitandaoni picha yangu na jezi ya Young Africans ikisambaa, ni kweli yule ni mimi na picha ile niliichapisha miezi kadhaa iliyopita hata kabla ya kudhani tutakutana na Simba.
“Hii ni baada ya kuona imefika mbali watu walinishauri niifute na mimi nilipokaa chini nikakubaliana na ushauri wao, ila naamini siku moja nitakuja kucheza Ligi ya Tanzania,” amesema Joshua Mutale.
Si mara ya kwanza kwa mchezaji wa Zambia kuonyesha mahaba kwa timu ya Tanzania, ikumbukwe kuwa, misimu kadhaa iliyopita, Moses Phiri akiwa Zanaco ya Zambia alikuwa akionekana amevalia jezi ya Simba ambayo alidai alikuwa akipelekewa na rafiki yake, Clatous Chama, lakini baadaye alijiunga na Simba rasmi.