Pacome Zouzoua Moto wa Kuotea Mbali Sana, Amtumia Salamu Jean Baleke

 


Kiungo Mshambuliaji wa Young Africans raia wa Ivory Coast, Pacome Zouzoua, amesema hatabweteka na mabao matatu aliyoyafunga katika Ligi Kuu Bara msimu huu, huku akipanga kuendelea na mwendelezo mzuri wa kufunga kwenye michezo ijayo.


Kauli hiyo huenda ikawa salamu kwa mshambuliaji wa Simba SC Mkongomarni, Jean Baleke ambaye ni kinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara akifunga mabao 5, akifuatiwa na Feisal Salum wa Azam FC mwenye mabao manne, huku Pacome, Stephane Aziz Ki, Maxi Nzengeli na Matheo Anthony wakifunga matatu kila mmoja.


Pacome amesema anafurahia mwanzo mzuri wa kufunga aliouanza katika ligi, ambapo amefunga mabao matatu kwenye michezo mitano, huku akipanga kufunga idadi kubwa ya mabao.


Kiungo huyo kwa sasa ni kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha Young Africans kinachonolewa na Kocha Muargentina, Miguel Gamondi.


Pacome amesema lengo la kufunga idadi kubwa ya mabao, ni kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki pamoja na ubingwa wa ligi msimu wake wa kwanza akiwa na timu hiyo.


Ameongeza kuwa, tayari ameizoea ligi, sasa alichobakisha ni kuthibitisha ubora wake kwa kuifanyia makubwa Young Africans ikiwemo kufunga na kutengeneza nafasi za mabao kwa wachezaji wenzake.


“Kila siku nafikiria kitu kipya cha kukifanya ninapokuwepo uwanjani, lengo ni kuona ninaendeleza mwendelezo mzuri niliouanza wa kufunga mabao matatu katika ligi.


“Haitakuwa kazi nyepesi kwangu kufunga mabao, kutokana na ubora wa wapinzani wetu tunaokutana nao, lakini kwa kushirikiana kwa wachezaji wenzangu nitafanya mengi makubwa.


“Ninataka kuthibitisha ubora wangu msimu huu ukiwa wa kwanza kwangu, lengo ni kuhakikisha tunatetea ubingwa wa ligi na kufika mbali Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema Pacome.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad