Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Paul Makonda, amesema kwa sasa anaomba kuelekezwa, kushauriwa na watendaji na watumishi pamoja na kwamba anahitaji kujifunza kutoka kwa viongozi waliowahi kushika wadhifa huo akiwemo Waziri wa Habari Nape Nnauye.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Oktoba 26, 2023, jijini Dar es Salaam mara baada ya kupokelewa rasmi kwenye ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba.
"Nitumie fursa hii kuwaomba watendaji na watumishi ushirikiano na kunifundisha, kunielekeza na kunishauri kwa uaminifu mkubwa ya kwamba taarifa mnazonipa ndiyo halisi hata wewe ungeifanyia kazi," amesema Makonda
Aidha makonda ameongeza, "Duniani kote watu wanaishi kwa taarifa, na taarifa ndiyo inafanya maamuzi, ukiwa na chanzo kibovu utafanya maamuzi mabovu, ukiwa na chanzo kizuri utafanya maamuzi sahihi, ni matarajio yangu mtanipa taarifa sahihi ili niweze kufanya kazi ya kumsaidia Katibu Mkuu wetu wa chama, Makamu wetu na Mwenyekiti wetu na hatimaye kwa pamoja kukiimarisha na kukijenga chama kwa wananchi,"
Mwisho atakatoa raia kwa wale waliomtangulia kwenye nafasi hiyo, "Nikuombe (Sophia Mjema) nahitaji kujifunza kwako, kwa Shaka Hamdu Shaka, nahitaji kujifunza kwa Polepole na Nape wale wote waliotangulia wanacho kitu cha kutoa mchango kwa chama chetu na mimi nitaendelea kugonga hodi kwenu na nitaomba sana mnifungulie milango,".