Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani wilayani Mbulu, Mkoa wa Manyara, limewataka abiria kuacha kushabikia madereva wanaoendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi kwani husababisha ajali.
Ofisa wa kikosi hicho wilayani Mbulu, Koplo Esther Mwijarubi ameyasema hayo jana Ijumaa Oktoba 20 wakati akitoa elimu ya wajibu na haki ya abiria wawapo barabarani Katika Kituo Kikuuu cha mabasi.
Mwijarabu ameeleza kuwa abiria kushabikia madereva wanaovunja sheria ni chanzo cha ajali, hivyo ni jukumu la kila mmoja kukemea vitendo hivyo na siyo kushabikia.
"Mnaposhabikia dereva anayeendesha bila kuzingatia kanuni na sheria ni hatari sana kwani husababisha ajali," amesema Mwijarubi.
Amewataka abiria kuachana na hali hiyo kwani ajali haina kinga ila isitafutwe kwa njia ya kushabikia mwendo kasi na kusababisha madhara kwao.
"Tabia ya abiria kushabikia mwendo kasi imekuwa ni chanzo kwa madereva kuvunja sheria na kusababisha ajali za mara kwa mara barabarani," amesema Mwijarubi.
Amesema jeshi la polisi, kikosi cha usalama barabarani wilayani Mbulu linawataka abiria, madereva na watumiaji wa barabara kutii na kuzingatia kanuni na sheria za usalama barabarani ili kuzuia ajali.
Mmoja kati ya abiria wa katika kituo hicho cha mabasi mjini Mbulu, Mateo Nada amepongeza juhudi za Polisi kutoa elimu kwani husaidia kupunguza ajali zisizo na ulazima wa kutokea.
"Baadhi ya abiria kushabikia mwendo kasi kwa madereva ni changamoto kubwa hivyo kitendo cha trafiki kukemea hali hiyo kinapaswa kupongezwa," amesema Nada.
Amesema elimu hiyo itolewe mara kwa mara ili matukio hayo yasijirudie kwa watu kushabikia mwendo kasi ili hali ndiyo chanjo cha ajali nyingi nchini kupitia vyombo vya moto.
Abiria mwingine Rose John amesema wanaoshabikia dereva aendeshe gari kwa kasi hakuna faida yoyote wanayopata zaidi ya kusababisha ajali na kwa watu kupoteza maisha au kujeruhiwa.
"Ni vyema elimu hii iendelee kutolewa ili ikomeshwe kwani ushabiki usiokuwa na faida kwa kushangilia mwendo kasi unapaswa kukomeshwa kwa kweli," amesema.