Rais Samia afichua siri ya kumteua Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu

 


Rais Samia Suluhu Hassan ameweka hadharani sababu ya kumteua Dk Doto Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kwamba ni utekelezaji wa agizo lake la kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya madini kwa muda mfupi kuliko aliompangia.


Alisema hayo jana jijini Dodoma, alipozindua mitambo ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo na mitambo ya Shirika la Madini Taifa (Stamico). Shirika hilo pia lilitia saini mkataba wa kufanya utafiti wa madini na utengenezaji wa mkaa mbadala.


Rais Samia alisema siku alipomuapisha Dk Biteko kuwa Waziri wa Madini, alimwambia walimpatia dhima ya kuhakikisha sekta hiyo ikifika mwaka 2025 ichangie Pato la Taifa kwa asilimia 10.


Hata hivyo, alisema Dk Biteko alifikisha kiwango hicho mwishoni mwa mwaka jana.


“Kwa hiyo ametumia muda mfupi kuliko tulivyomkadiria. Sasa nikaona mbinu ileile aliyoitumia kule nimpandishe awe Naibu Waziri Mkuu aje atusaidie huku. Lakini nimkabidhi na Nishati pia aende atusaidie huku. Kwa hiyo Dokta hongera na pole,” alisema Samia.


Katika hatua nyingine, akiwazungumzia wachimbaji wadogo wa madini, Rais Samia alisema wamekuwa wakifanya shughuli zao bila kuwa na taarifa za kiikolojia, jambo linalosababisha wafanye uchimbaji wa kubahatisha. Alisema hali hiyo imewafanya kushindwa kukopesheka na kukosa taarifa madhubuti za uwepo wa mashapo.


“Ili kutatua changamoto hiyo Waziri wa Madini (Anthony Mavunde), ameeleza vizuri mpango wa Serikali ambao ni sehemu ya dira ya mwaka 2030 unaoelekeza kufanya utafiti wa madini kwa kutumia teknolojia ya kisasa ifikapo mwaka 2030 au mapema itakavyoweza,” alisema.


Alisema mpango huo utatekelezwa katika eneo kubwa ili Tanzania iboreshe taarifa za kiikolojia zilizopo. Kwa sasa eneo lililopimwa ni asilimia 16 tu ya nchi nzima.


“Hapa ndipo tunaposema tuna utajiri lakini tumeukalia, sababu tumepima eneo dogo na ndilo tunalolitumia, lakini matokeo yake ni makubwa. Tukienda mara mbili zaidi ya asilimia 16, nchi hii matokeo yake hatutakuwa na mikopo na hatutakuwa na upungufu katika bajeti zetu,” alisema.


Alisema upatikanaji wa taarifa hizo utasaidia kuwa na viashiria vya madini kwenye miamba kwa maeneo mbalimbali, hivyo kuwezesha utafiti wa kina kufanyika.


Katika utekelezaji wa mpango huo, jana Rais alizindua mitambo mitano yenye thamani ya Sh2.73 bilioni, ambayo iko tayari kufanya kazi katika maeneo ya wachimbaji wadogo.


Alisema mitambo hiyo itawapunguzia gharama wachimbaji wadogo ambao kwa sasa wamekuwa wakikodi na kulipa Sh300,000 kila wanapochoronga miamba.


Rais Samia aliwaonya wanaotorosha madini, akiwataka wafanyabiashara kuyauza katika viwanda vilivyopo nchini. Waziri Mavunde alisema eneo la asilimia 16 lililofanyiwa utafiti kwa mwaka wa fedha 2022/23 lilichangia upatikanaji wa fedha za kigeni kwa zaidi ya asilimia 56.


“Mauzo ya nje kwa sekta ya madini ni Dola za Marekani 3.3 bilioni, sawa na asilimia 56 ya mauzo ya bidhaa ya nje,” alisema Samia.


“Katika mwaka uliopita kwenye hilo eneo la asilimia 16 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya mapato ya ndani Sh2 trilioni, sawa na asilimia 15 iliyotoka kwenye sekta ya madini.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad