Samia aitisha NEC ya dharura CCM





Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ameitisha mkutano wa dharura wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) huku ikiaminika anaweza kuja na jambo jipya ndani ya chama hicho tawala.

Kikao hicho ambacho ajenda zake hazijatajwa, kimeitishwa ikiwa ni siku chache kabla ya muda wa kikao cha kawaida cha kikatiba, ambacho kinatarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Pia limeitishwa zikiwa zimepita siku 22 tangu kufanyika kikao cha kamati kuu ya chama hicho, ambacho pamoja na mambo megine, kilifanya uteuzi wa viongozi mbalimbali.

Katika uteuzi huo uliofanyika Oktoba mosi, Jokate Mwegelo, kuwa Katibu Mkuu wa UWT na Fakii Lulandala kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa UVCCM.


Licha ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Annamringi Macha kusema ndani ya chama hicho hakuna kikao kilichoitishwa jijini Dodoma, vyanzo mbalimbali, wakiwemo wajumbe wa NEC vimelieleza Mwananchi kikao hicho cha dharura kimeitishwa Oktoba 22 mwaka huu.

“Hakuna kikao chochote ndani ya chama kilichoitishwa na mtu yeyote hapa Dodoma, nakuhakikishia hakuna kikao na mtaona hivyo, niamini mimi nakuambia,” alisema Macha.

Macha alitoa kauli hiyo alipoulizwa swali kuwa, ni kikao kipi kati ya NEC na Kamati Kuu (CC) ambacho kimeitishwa jijini Dodoma.


Vyanzo vyetu vimelithibitishia gazeti kuwa kikao hicho kimeitishwa na mwenyekiti mwenyewe huku wengine wakidai, yalikuwa mawasiliano ya moja kwa moja bila kupitia sekretarieti.

CCM ina vikao vya aina tatu, vikao vya kikatiba vinavyoitishwa kwa mujibu wa kalenda na kuandaliwa ajenda kupitia sekretarieti ya chama.

Pia, kuna kikao maalumu ambacho huitishwa kwa jambo maalumu kinachoandaliwa na sekretarieti, kupangwa muda na wajumbe kupewa ajenda.

Kikao kingine ni cha dharura ambacho ajenda anakuwa nayo mwenyekiti au kwa kushirikiana na makamu wenyeviti, Zanzibar na Bara na wakati mwingine hata sekretarieti haihusishwi.


Kikao ya dharura

“Maana ya mkutano wa dharura ni pale unapoitishwa kwa jambo linalohitaji uamuzi wa haraka, lakini kwa kupitia vikao,” alisema Spika mstaafu Pius Msekwa, makamu mwenyekiti wa CCM-Bara mstaafu ambaye pia amewahi kuwa mtendaji mkuu ndani ya chama.

Msekwa alisema hata Bunge limewahi kuitisha mkutano wa dharura kujadili jambo muhimu.

“Wakati wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Bunge halikuwa kwenye ratiba, lakini lililazimika kuitishwa kwa dharura kujadili jambo hilo kwa ajili ya kutoa uamuzi kutokana na uharaka wake,” alisema Msekwa.

Chanzo kingine ndani ya CCM kiliungana na tafsiri ya Msekwa kikisema “mkutano wa dharura unapoitishwa anayefahamu ajenda ni mwenyekiti na wasaidizi wake wawili, makamu mwenyekiti Zanzibar na makamu mwenyekiti-Bara kwa kuwa wao NEC haiwagusi.


“Hakuna mtu anayejua ajenda zaidi ya mwenyekiti na makamu wenyeviti wake wawili peke yao. Ajenda anakwenda nazo mwenyewe maana ni kikao ambacho hakijaandaliwa na kamati kuu. Kwa wanaojua ni ya nini ni hao watatu peke yao, basi.

“Kwa hiyo wanaojua ni NEC ya nini ni mwenyekiti na makamu wenyeviti wake wawili. Hata katibu mkuu ambaye ndiye mtendaji mkuu wa CCM inawezekana akawa hajui,” kilisema chanzo chetu.

Kwa mujibu wa chanzo hicho miongoni mwa mambo yanayoweza kusababisha kuhitaji kikao cha dharura cha NEC, ni kama kuna majanga, mfano kama mafuriko, kimbunga kilichoathiri nchi au kuna jambo chama kinataka kuiambia Serikali au hata mabadiliko ya uongozi ndani ya chama.

“Ndiyo maana hisia nyingine hata ndani ya CCM yenyewe zinakuja, kwamba anataka kubadili sekretarieti ya Taifa kuelekea mwaka 2024 na 2025.

“Sina hakika NEC hiyo ya dharura itakuja au inaweza kuja na mabadiliko ya sekretarieti. Inawezekana au isiwe hivyo maana anayejua ajenda ni mwenyekiti peke yake, lakini itakuwa lazima amewashirikisha makamu wake maana ndio wasaidizi wake wakuu na kwa dhamana zao hawawezi kuguswa na kikao hicho,” kilisema chanzo chetu.


Chanzo kingine kilidokeza gazeti hili kuwa NEC hiyo huenda ikagusia suala la mkataba wa uwekezaji na uendelezaji wa Bandari Tanzania baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai kupitia kampuni yake ya DP World.

NEC ilipokutana Julai 9, 2023 iliubariki na ikisema “uwekezaji na uendeshaji wa bandari ni kwa manufaa ya uchumi wa nchi.”

Katika taarifa yake, ilisema “Uwekezaji huo ni utekelezaji wa vitendo wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025, ibara ya 59, ukurasa wa 92. Serikali iongeze kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo katika makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji huo wa bandari.”

Baada ya hatua hiyo, viongozi wa chama walisambaa nchini kutoia elimu, na chanzo cheti kinasema huenda NEC inakaa kufanya tathmini kabla ya utekelezaji wa mkataba huo kuanza.

Mkataba huo ilioridhiwa na Bunge Julai 10 mwaka huu uliibua mjadala mkali kwa umma na wanaharakati walifungua kesi kuupinga bila mafanikio.

Mabadiliko ya uongozi

Mbali na siala la mkataba, pia vyanzo vyetu vimetaja masuala mengine yanayozekana kujadiliwa ni mabadiliko ya uongozi katika ngazi mbalimbali.

Ukiacha Mwegelo na Lulandala, hivi karibuni CCM ilifanya uteuzi wa baadhi ya makatibu wakuu wa mikoa kwa kuteua wapya baada ya baadhi kustaafu na wengine walibadilishwa majukumu ya kazi, hali inayoashiria huenda kuna mabadiliko zaidi.

Katika mabadiliko ya karibuni, aliyekuwa katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Shaibu Akwilombe aliteuliwa kuwa Katibu Msaidizi Mkuu, Idara ya Itikadi na Uenezi ambayo ilikuwa wazi tangu Januari mwaka huu.

Akwilombe amechukua nafasi ya Zakaria Mwansasu aliyeteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Uyui, Tabora.

Pia, Saad Kusilawe aliyekuwa mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi, CCM Makao Makuu amekuwa katibu msaidizi mkuu wa Idara ya Organaizesheni iliyokuwa wazi kuanzia Januari mwaka huu.

Kusilawe amechukua nafasi ya Solomon Itunda aliyeteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Songwe, Januari mwaka huu.

Pia, Eva Degeleki aliyekuwa ofisa utumishi, Idara ya Utawala na Uendeshaji Makao Makuu, aliteuliwa kuwa katibu wa CCM wa Mkoa wa Simiyu.

Selemani Sankwa aliyekuwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Tanga ameteuliwa kuwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Tanga.

Ibrahim Mjanaheri aliyekuwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Moshi Mjini, ameteuliwa kuwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Mara.

Pia, Idd Mkowa aliyekuwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Arusha Mjini, ameteuliwa kuwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Manyara.

Saidi King'eng'ena aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Siasa na Organaizesheni Makao Makuu ya Umoja wa Wazazi, Dodoma ameteuliwa kuwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Songwe.

Pia, Odilia Batimayo aliyekuwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Mbogwe, Mkoa wa Geita ameteuliwa kuwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga.

Bernard Ghati aliyekuwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kibaha Vijijini, ameteuliwa kuwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Pwani.

Pia, Marco Mbanga aliyekuwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Pwani, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Utawala, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu, Lumumba, Dar es Salaam kuchukua nafasi ya Rehema Msengi aliyeteuliwa kwa Katibu wa Wilaya ya Ilemela, Mwanza

Teuzi hizi pia zilikwenda sambamba na za makatibu wa CCM wa wilaya wapya, makatibu wa Jumuiya wa wilaya na mabadiliko ya vituo vya kazi kwa baadhi ya watendaji wa ngazi zilizoguswa na teuzi hizo.

Mitazamo ya wachambuzi

Mchambuzi wa masuala siasa, Dk Leons Mjwahuzi alisema endapo kikao hicho kitafanyika kina kinaweza kuwa na mabadiliko kwa kuwa ni jambo la kawaida kwa kiongozi mkubwa kufanya mabadiliko kila anapoona inafaa.

Hata hivyo, alisema mabadiliko katika maeneo mengi yanategemewe kutokea hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.

Dk Mjwahuzi alisema mara baada ya Rais Samia kuchukua kijiti cha uongozi wa CCM, kuna mambo aliendelea kujifunza ambayo kwa sasa si mgeni nayo kwenye uongozi, maana itamlazimu kufanya mabadiliko ili yaendane na matakwa yake.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema kikao cha dharura lazima kitakuwa na jambo maalumu, kwa hiyo wananchi wategemee kusikia mabadiliko.

Dk Loisulie alisema jambo la dharura haliwezi kusubiri kikao cha kikatiba, badala yake linafanyika wakati wowote inapobidi kufanyika ili mradi kipatikane kinachotafutwa.

Alisema kwa namna yoyote kama hakutakuwa na mabadiliko ya kiuongozi basi kutakuwa na jambo nyeti linalojadiliwa kwa masilahi ya nchi na Watanzania.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad