Joto linaloendelea kuhusu Diamond kuonekana kumtenga na kumsusa waziwazi mwanawe na Hamisa Mobetto huenda halitapoa muda wowote hivi karibuni kwani sasa limefikia mpaka vyombo vya dola.
Baada ya watu mbalimbali mitandaoni kumtaka Diamond kuwajibika kwa kukubali vipimo vya hadharani vya DNA ili kubaini iwapo mtoto huyo anayemtenga ni wake kweli ama ni wa kubabatizwa, sasa waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia na wanawake na makundi maalum, mheshimiwa Dorothy Gwajima amekuwa kiongozi wa serikali wa hivi karibuni kuliweka sakata hilo kwenye mizani.
Waziri Gwajima katika moja ya majibizano yake na shabiki mitandaoni, shabiki huyo alimtaka kuvunja ukimya kuhusu sakata hilo ambalo kwa asilimia kubwa linaonekana kuegemea moja ya majukumu yanayofaa kutelekezwa na wizara yake.
Shabiki huyo alimwandikia kwamba;
“Hivi wewe waziri si ndio mwenye dhamana ya kulinda watoto nchi hii, kinachoendelea mitandaoni kuhusu Dylan kunyanyasika mitandaoni huoni? Mbona unashindwa kuutatua huu mzozo? Muite Diamond kwa muda wake na Hamisa kwa muda wake uongee nao. Kama DNA ifanyike ili mtoto aache kunyanyasika mitandaoni, mbona kama huoni mtoto ananyanyasika kisaikolojia,” shabiki huyo alimburuza waziri.
Waziri huyo alimjibu shabiki huyo kuhusu sakata hilo alimwambia;
“Unajua huduma za jamii tumesogeza karibu na jamii kama zilivyosogezwa huduma nyingine zote? Hivyo hawa wazazi kama wana mgogoro wowote mahala sahihi sio mtandaoni bali ni kwenye huduma za ustawi wa jamii, halimashauri au mkoa au kituo chochote cha polisi karibu nao. Dawati la jinsia lakini pia tuna namba 116 ya dharura zote kuhusu masuala ya watoto na jamii,” waziri alijibu.
Sakata la Diamond kumsusa mwanae lilipata kuchochewa Zaidi wiki jana baada ya msanii huyo kuwakusanya wanawe wote kutoka kwa kina mama aliozaa nao kasoro Dylan wa Hamisa na kwenda nao Rwanda.
Mashabiki walicharuka vibaya wakisema kwamba kitendo anachokifanya ni kumhukumu mtoto kwa kosa ambalo halijui.