Sintofahamu Bosi wa 'Mwendokasi'





Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku nane kuisha tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aipe siku 12; Kampuni ya Uendeshaji Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), kutengeneza mabasi 70 yaliyoharibika, Mkurugenzi wake, John Nguya ametumbuliwa.

Oktoba 12, Chalamila alifanya ziara katika kituo cha mabasi hayo cha Kimara na Mbezi, ikiwa ni siku moja baada ya Mwananachi kuripoti changamoto wanazopitia abiria katika kupata huduma ya usafiri huo.

Pamoja na mambo mengine, Chalamila katika maagizo yake alitoa siku 14 (wiki mbili), kwa Udart ambao ndio wasimamizi wa uendeshaji mabasi hayo kuyatengeneza mabasi 70 ambayo yameharibika ili kuwapunguzia adha wananchi wanaotumia usafiri huo.

Katika ziara yake hiyo, Chalamila aliongozana na viongozi mbalimbali wakiwemo wa kisiasa, Wilaya ya Ubungo pamoja na Wakala wa Mabasi yaendao Haraka (Dart), ambao ni wasimamizi wa mradi huo upande wa Serikali.


Maagizo aliyoyatoa

Katika maagizo yake, Chalamila amesema mtoa huduma anapaswa kutengeneza magari hayo 70 huku akisema anaingiza mapato kutoka na kazi ya usafirishaji, na kwamba anashangaa kwa nini kuna idadi kubwa ya mabasi ni mabovu.

"Baada ya wiki mbili nataka kuona magari hayo yote yanarudi barabarani ili kuwapunguzia adha ya usafiri wananchi.

Sitakuwa tayari kuona Rais Samia Suluhu Hassan aliye na nia njema na juu mradi anatukanwa, kwa sababu tu ya uzembe wa watu fulani kushindwa kutimiza majukumu yao,” aalieleza Mkuu huyo wa mkoa.


Pia aliongeza kuwa wataendelea kufuatilia utoaji wa huduma, na kama hakutakuwa na mabadiliko watalazimika kufanya mabadiliko ikiwemo kumuweka pembeni mwekezaji aliyepo.

Kutumbuliwa kwa Mkurugenzi Udart

Hata hivyo wakati siku 14 zikiwa hazijaisha, taarifa ambazo Mwananchi imezipata ni kwamba aliyekuwa Mkurugenzi wa Dart, John Nguya, ameondolewa kimyakimya na nafasi yake kuchukuliwa na aliyewahi kuwa bosi wa Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra).

Taarifa hizo za uhakika, zinasema bosi huyo mpya ameanza kuripoti kazi kuanzia jana (Jumatatu), licha ya kuwa wafanyakazi bado hawajatangaziwa rasmi.

“Ni kweli tuna bosi mpya, tumemuona kuanzia jana akiwa ofisini, lakini hatujatangaziwa bado rasmi,” kimesema chanzo hicho ambacho hakikuwa tayari jina lake kutajwa.


Mwananchi ilimtafuta Msemaji wa Udart, Catherine Mtao, kuweza kulizungumzia hilo ambaye hakukubali wala kukataa kuhusiana kuwepo kwa mabadiliko hayo ya uongozi isipokuwa alimtaka mwandishi aandike barua na kuifikisha ofisini kwao kwa ajili ya kupatiwa majibu.

“Utaratibu wetu inakupaswa kuandika barua ili tuweze kukujibu unachotaka na ni maelekezo kutoka kwa bosi wangu, hivyo nashauri ufanye hivyo ili upate unachohitaji kujua kutoka kwetu,”amesema Catherine.

Kwa upande wa Nguya, alipotafutwa na Mwananchi Digital kuthibitisha juu ya habari hizi, amejibu kwa kifupi akisema yeye sio mzungumzaji wa mradi hivyo watafutwe Dart wanaweza kuwa na majibu ya suala hilo.

Mwandishi wetu alipotaka kujua kama kweli kaondolewa katika nafasi yake, Nguya amesisitiza: “Nimeishakuambia kuwa mimi kwa sasa sio msemaji wa Udart, naomba uwatafute wahusika niliokuelekeza.”


Kwa upande wa Dart, alipotafutwa msemaji wake Willium Gatambi, simu yake iliita kidogo na kisha kukata, na baadaye ya muda kidogo, alituma ujumbe wa maandishi uliosomeka: ”Sorry, I cant’t talk right now’ (Samahani, kwa sasa sitaweza kuongea).


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad