Kocha mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema maandalizi kuelekea mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam Fc utakaopigwa leo Jumatatu, Oktoba 23, 2023 katika Dimba la Mkapa yamekamilika.
Gamondi amesema vijana wake wako tayari kwa mechi nne mfululizo za Ligi ukiwemo mchezo wa kesho dhidi ya Azam Fc na malengo ni kushinda.
"Tunafahamu tunakwenda kupambana na timu ngumu Azam Fc, moja ya timu bora hapa Tanzania lakini sisi tuna malengo ambayo tunahitaji kuyatimiza.
"Nafurahi tumerejea katika uwanja wa Benjamin Mkapa, hari ya kikosi iko juu, kila mmoja ana shauku kubwa ya kucheza mchezo huo.
"Zipo changamoto za majeruhi, kuna wachezaji watatu ambao wana majeraha madogo lakini nafikiria baada ya mazoezi ya mwisho leo tutakuwa na wachezaji 20 kwaajili ya mchezo huo," alisema Gamondi
Gamondi amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi katika dimba la Benjamin Mkapa kuishangilia timu yao kwani anaamini shabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake winga Skudu Makudubela amewataka mashabiki wa Yanga wajitokeze kwa wingi uwanjani kwani wamewaandalia burudani itakayoambatana na ushindi mnono
"Kama kocha alivyosema tunawahitaji mashabiki waje uwanjani kwa wingi kwani wao ni wachezaji wa 12. Tunafahamu wachezaji wetu wanahitaji burudani ambayo ni kushangilia magoli hivyo tunawaahidi tutawapa burudani hiyo," alisema Skudu