Kocha wa Coastal Union, Mwinyi Zahera amewasilisha barua rasmi ndani ya uongozi wa timu hiyo ya kuelezea sababu ya kikosi hicho kuanza vibaya msimu huu na hii ni kutokana na uwepo wa taarifa zinazomuhusu kuzuiwa kujiunga na kambi.
Hilo linajiri baada ya viongozi wa klabu hiyo kumzuia kutojiunga na kambi ya timu iliyokuwa jijini Mbeya kwa ajili ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu utakaopigwa Jumamosi hii ya Oktoba 21, kwenye Uwanja wa Highlands Estate.
Akizungumza na Mwanaspoti Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Abbas Elsabri alisema hawezi kuweka wazi juu ya taarifa hizo hadi pale atakapopata ukweli kutoka kwa viongozi ambao ndio wana jukumu kubwa la kumpatia ili yeye aweze kuzitoa kwa umma.
"Kama zipo basi sisi tutaweka wazi ila kwa sasa tambua tu kwamba tunaendelea na maandalizi yetu kwa ajili ya mchezo na Ihefu, lengo ni kupata matokeo mazuri kwa sababu ukiangalia tulivyoanza msimu ni tofauti na malengo yetu," alisema.
Wakati Elsabri akizungumza hayo ila Mwanaspoti linatambua Zahera amewasilisha barua ya kueleza kwanini timu hiyo haina matokeo mazuri tangu msimu umeanza kutokana na kucheza michezo mitano ya Ligi Kuu Bara bila ya kupata ushindi wowote.
Wakati Zahera amewasilisha ripoti yake ila Mwanaspoti linatambua kwa sasa kikosi hicho kitakuwa chini ya Kocha Msaidizi, Fikiri Elias huku viongozi wakimuongezea nguvu na staa wa zamani wa klabu hiyo akiwemo, Razak Yusuf maarufu 'Kareka'.
Katika michezo mitano aliyoiongoza kikosi hicho Zahera ametoa sare miwili na kupoteza mitatu huku ikiwa mkiani na pointi zake mbili tu.