Timu Mpya ya Mbwana Samatta Noma Ulaya, Wapo Nafasi Nzuri Kutinga Makundi
PAOK FC anayoichezea Mtanzania Mbwana Samatta imejiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya 16 bora ya mashindano ya Uefa Conference League baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Eintracht Frankfurt.
Bao la jioni la Konstantinos Koulierakis lilitosha kuipa ushindi PAOK katika mchezo huo ambao umeifanya iendelee kukamata uongozi wa kundi G la mashindano hayo, ikifikisha pointi sita huku Franfurt ikifuatia ikiwa na pointi tatu.
Koulierakis alifunga bao hilo baada ya kuunganisha mpira uliombabatiza mgongoni mchezaji wa Frankfurt, Makoto Hasebe ambao ulitokana na faulo iliyopigwa na Stefan Schwab.
Ilionekana kama mchezo huo ungemalizika kwa sare ya bao 1-1 baada ya dakika ya 68, Omar Marmoush wa Frankfurt kusawazisha bao la dakika ya 28 la Andrija Zivkovic, lakini bao la Koulierakis likapeleka furaha kwa PAOK.
Na habari nzuri zaidi kwa timu hiyo ya Samatta ikawa ni sare ya bao 1-1 ya wapinzani wao wengine kwenye kundi hilo, Aberdeen na HJK Helsinki.
Katika mchezo uliopigwa leo usiku, Samatta alianza kikosini na kucheza hadi dakika ya 85 alipotolewa kisha nafasi yake kuchukuliwa na Brandon Thomas na nahodha huyo wa Taifa Stars, alifunga bao lililokataliwa katika dakika ya 16 kwa kile kilichotafsiriwa na mwamuzi kuwa aliotea.
Matokeo hayo yanaifanya PAOK ihitaji pointi nne tu katika mechi nne zilizosalia za kundi hilo ili iweze kuingia hatua ya 16 bora.
Kwa upande mwingine, ushindi umeifanya PAOK iwe na mwendelezo wa kupata matokeo mazuri katika siku za hivi karibuni katika mashindano ambayo inashiriki.
Timu hiyo tangu ilipofungwa bao 1-0 na OFI katika Ligi Kuu Ugiriki, imecheza mechi sita mfululizo za mashindano tofauti bila kupoteza ikishinda nne na kutoka sare mbili.