Tundu Lissu aeleza sababu za kwenda Marekani




Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)-Bara, Tundu Lisu ameweka wazi sababu za yeye kuwepo nje ya nchi baada ya kuhitimisha mikutano ya hadhara iliyofanyika Kanda ya Ziwa.

Agosti 2023, chama hicho kikiongozwa na Mwenyezi wake, Freeman Mbowe, kilifanya ziara kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa ikijulikana Operesheni +255 Katiba Mpya. Mara baada ya kumalizika, Lissu akwenda nchini Marekani.

Jana Jumamosi, Oktoba 21, 2023 akizungumza akiwa nchini Marekani kwenye kipindi cha Medani za Siasa kinachorushwa na Star tv, Lissu alisema, alikwenda nje ya nchi kwa mambo mawili ikiwemo kupumzika baada ya kumaliza mikutano kwani alikuwa amechoka sana.

Alisema alifanya kazi kubwa kwa mfululizo hivyo alihitaji kupumzika na sababu ya pili ni ya kikazi kwani amekuwa akifanya utafiti kwa muda mrefu kuhusiana na masuala ya mfumo wa uchaguzi.


"Niliondoka ili kumalizia kazi hiyo ya utafiti masuala hayo ya mfumo wa uchaguzi nilitaka kukaa sehemu bila mtu yoyote kuniona, kunipigia simu wala kuniambia habari hii wala ile," alisema Lissu

Akizungumzia sababu ya kuondokea nchini Kenya alisema, alimaliza mkutano wake wa mwisho Arusha ambapo kuondoka hapo hadi Nairobi ni saa nne hivyo ni karibu kuliko akwenda jijini Dar es Salaam.

"Ningesafiri hadi Dar es Salaam ni mbali na kuongeza gharama zisizokuwa na sababu yoyote, ilikuwa ni rahisi kupitia mpaka wa Namanga," alisema


Aidha, Lissu alisema kuna shirika ambalo anafanya nalo kazi anaweza kufanyia kazi mahali popote hivyo hata akiwa Marekani anaweza kufanyia hukohuko.

Kuhusu mfumo wa uchaguzi alisema mfumo huo ni mbovu kila eneo linahitaji marekiebisho.

"Hatuzungumzii uteuzi na upatikanaji wa wagombea, uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu uliopita wagombea walienguliwa lakini mfumo wa kampeni ni matatizo matupu," alisema

"Siku ya uchaguzi wenyewe ni matatizo vitu gani vinapaswa kufanyika pia mfumo wa kuhesabu kura na kutangaza matokeo ni matatizo matupu nikianza kuelezea mfumo mzima wa uchaguzi nitahitaji siku tatu," alisema na kuongeza.


Kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi Lissu alisema, kama wangekuwa wanasimamia sheria watu wengi wanaowapigia saluti wangetakiwa kuwa gerezani.

Alisema Jeshi la Polisi wajibu wake mkubwa ni kuhakikisha walioko madarakani wanaendelea kuwepo madarakani.

"Kinachotakiwa ni kwamba yafanyike yale mambo ambayo yameshauriwa na tume mbalimbali, Jeshi la Polisi linahitaji Mapinduzi ya kweli kubadilisha mfumo mzima," alisema

"Jeshi la Polisi linatakiwa lifunguliwe kwenye kifungo cha kisiasa ambacho limekuwa likifungiwa kwa muda mrefu, tatizo kubwa limekuwa likiingiliwa na mamlaka za kisiasa ikiwemo wakuu wa mikoa na wakuu wa Wilaya,"alisema.


Lissu ambaye alikuwa mgombea Uraisi katika uchaguzi mkuu wa 2020 alisema kunahitajika mabadiliko makubwa katika Jeshi la Polisi ikiwemo kuondoa udhibiti wa kisiasa.

"Rais na Waziri wa Mambo ya Ndani, uhusiano wao unapaswa kuwa kwenye sera tu, Serikali inatengeneza sera na sheria masuala yote yanayohusiana na Jeshi la Polisi bila kuingiliwa na mamlaka za kisiasa kwenye masuala ya kiutendaji," alisema

"Wakuu wa mikoa na Wilaya hawana utaalamu wowote kwenye masuala ya ulinzi na usalama, kinachotakiwa ni kuondoa mamlaka za kisiasa juu ya Jeshi la Polisi ili kuondoa nguvu waliyonayo ya kuwasaidia wananasiasa kuendelea kutawala,"

Lissu ambaye pia ni mwanasheria alisema kuna haja ya kufanyika mabadiliko kuanzia kwenye sheria kwani hakuna sababu ya Rais kumteua Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) pekee yake.

Alisema hakuna sababu ya IGP kuwateua Makamanda wa Polisi wa Mikoa, kwani nchi nyingine huteuliwa na mameya kufanya hivyo kutawafanya wawajibike kwa wananchi wao.


Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime akizungumza na Mwananchi Digital juu ya madai aliyoyatoa Lissu alisema, Jeshi la Polisi limeundwa na kupewa majukumu na sheria mama.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi wasaidizi Sura ya 322 miongoni mwa majukumu hayo ni kulinda maisha ya watu na mali zao, kubaini kuzuia, kutanzua uhalifu kukamata na kupeleleza wanaojiandaa na waliotenda makosa ya uhalifu wa kijinai.

"Hivyo Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo na ndiyo maana nchi yetu inaendelea kuwa ya amani, utulivu,upendo,usalama na mshikamano," alisema Misime.

Misime alisisitiza Jeshi la Polisi litaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kufuata sheria za nchi atakayekiuka sheria au atakayeonyeshe viashiria vyovyote vya kutaka kuvunja sheria au kuvuruga amani ya nchi kwa kisingizio chochote kile atachuliwa hatua kama sheria inavyoelekeza kwani hakuna aliyej uu ya sheria.

Katika mahojiano ya Lissu, aliweka bayana kauli aliyoitoa kuhusiana na kuvunjika kwa maridhiano baina ya Chadema na Chama cha Mapinduzi alieleza kuwa chama hicho kilikataa.

Alisema mapendekezo yao juu ya mabadiliko ya Katiba, mfumo wa uchaguzi na kuondolewa kwa sheria za uchaguzi vyote wamevikataa kwa maandishi.

"Mwenyekiti akiwa Zanzibar kwenye sherehe za maadhimisho ya siku wazee akizungumza kuwa CCM wamekata mapendekezo yetu, hatujakataa wala hatujavunja maridhiano wamekataa," alisema



Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad