Unyama ni Mwingi wa Simba Leo kwa Mkapa

Unyama ni Mwingi wa Simba Leo kwa Mkapa


Kwa lugha rahisi ya mtaani ni kwamba leo unyama ni mwingi. Heshima itaandikwa kwenye Uwanja wa Mkapa Simba itakapowakabili Al Ahly. Ukiachana na wageni wengine wakubwa, Kwa mara ya kwanza leo, Kocha mwenye heshima kubwa kwenye soka la Ulaya, Arsene Wenger atakuwa Kwa Mkapa akiangalia boli.


Ni Kocha mkubwa aliyeweka heshima akiwa na Arsenal na anaheshimika kwenye Ligi Kuu ya England. Atashuhudia unyama mwingi Kwa Mkapa.


“Kila mpinzani lazima aiheshimu Simba, kwa kuwa ina mastaa wakubwa, ina kikosi bora,”hii ni kauli ya kocha wa Simba, Olivier Robert Robertinho, akizungumza na nasi jana muda wa lanchi Jijini Dar es Salaam.


Leo dunia ya soka itahamia Tanzania katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Ni katika uzinduzi wa michuano mipya ya African Football League ambapo pamoja na shamrashamra za ufunguzi wake, kutapigwa mechi ya kiume kati ya Simba na Al Ahly kutoka Misri.


Simba imekuwa timu tishio kwa siku za hivi karibuni, ikiwa imefanya makubwa kwenye soka la Afrika, Shirikisho la Soka Afrika (Caf) iliitangaza kuwa timu ya saba kwa ubora baada ya kufika robo fainali mara tatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa na mara moja Kombe la Shrikisho..


Katika michezo tisa iliyopita kwenye michuano yote, Simba haijapoteza hata mmoja ikiwa imeshinda saba na kutoka sare miwili. Simba ushindi asilimia 100


Al Ahly, ambao walitua nchini na mkwara mzito juzi usiku, hawajapoteza kwenye michezo yao mitano mfululizo, hii inaonyesha kuwa wanaume wa kweli wanakwenda kukutana kuwania ubingwa wa michuano mipya kabisa Afrika lakini yenye fedha nyingi ikionyeshwa Live kwenye Tv ya Fifa tena bure. Hilo ni la kwanza kutokea kwa timu za ukanda huu.


Simba wamekuwa bora wanapocheza na Ahly Kwa Mkapa, wakiwa wamekutana nao mara nne na kupata ushindi wa asilimia 100, yaani walishinda michezo yote na huu utakuwa mchezo wa tano wanakutana. Siyo mechi ya kitoto.


Katika mchezo huu Simba wanakuwa na kiburi kutokana na kuwa na mastaa wanaofahamu jinsi ya kucheza michezo hii, uwepo wa beki Enock Inonga anayecheza timu ya Taifa ya Congo, Clatous Chama anayecheza Zambia, Che Malone Fondoh ambaye alicheza dhidi ya Al Ahly msimu uliopita akiwa na Cotton Sport, bila kumsahau, Mohamed Hussein, Shomary Kapombe na Aishi Manula ambao siyo wageni kwenye shoo kama hizi, hawa wanapewa nafasi kubwa zaidi ya kuhakikisha ushindi unabaki nchini.


Mara nyingi Simba wamekuwa na kasi kubwa wanapocheza dhidi ya Al Ahly na leo inaonekana ndiyo itakuwa nguzo yao kubwa, ili kuwachanganya mastaa wao kama Percy Tau ambaye anatajwa kuwa mchezaji anayelipwa ghali zaidi Afrika.


Udhaifu kipa Ahly:


Akili kubwa na pekee ambayo Simba wanaweza kuitumia ili kupata mabao mengi ni kupiga mashuti ya mbali ambayo yamekuwa yakimshinda kipa wa Ahly, Mohammed El Shenawy, kumbukumbu zinaonyesha kuwa ni kati ya vitu ambavyo vinamsumbua.


Katika mchezo wa msimu uliopita dhidi ya Mamelodi aliruhusu mabao mawili kwa mashuti ya nje ya 18, lakini mchezo uliopita kwenye Uwanja wa Mkapa ambao Simba ilishinda bao 1-0 aliruhusu pia bao la aina hiyo, lilowekwa kimiani na Luis Misquissone ambaye leo amepania haswa na alifanya mazoezi spesho.


Hata hivyo, upande wa Tshabalala, Simba watatakiwa kupawekea mkakati maalum kwa kuwa ni eneo ambalo staa Pecy Tau amekuwa akipatumia zaidi, lakini akiwa mchezaji mwenye kasi zaidi kwenye timu hiyo na kama Anthony Modeste waliomsajili kutoka Borrusia Dortmund atakuwepo basi Simba watatakiwa kuhakikisha wanaweka eneo lao la ulinzi badala ya kwenda na mfumo waliouzoea.


Modeste Raia wa Ufaransa ni kati ya washambuliaji mahiri akiwa na uwezo wa kupiga mashuti makali ya nje ya eneo la 18 la timu pinzani.


Simba kwenye mchezo huu pamoja na kutafuta ushindi itakuwa sehemu ya kuonyesha ukubwa wao kama alivyosema kocha wa Ahly, Marcel Koller: “Kila anayecheza nasi mechi yake inakuwa maarufu zaidi, tumejiandaa kwa ajili ya mchezo huu kikamilifu na tunafahamu tunakutana na timu bora.”


Kama ilivyo kwa Kapombe na Tshabalala, Ahly nao wanawatumia Ali Maaloul na Mohammed Hany kama mabeki wa pembeni, wanauwezo zaidi wa kutengeneza nafasi kuliko kufunga, jambo ambalo kama Simba wakilitumia eneo hili wanaweza kupata mabao.


Michuano yenyewe:


Michuano hii imelenga kukuza, kurithisha na kulipa thamini kubwa soka la Afrika ambapo katika msimu wake wa kwanza ambao unazinduliwa rasmi leo itahusisha timu nane pekee, ambazo zimechaguliwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ubora na umaarufu wa klabu lakini kwa msimu utakaofuata timu zitaongezeka na kuwa 22.


TIMU SHIRIKI


Msimu huu ni Al Ahly SC (Misri), Enyimba FC (Nigeria), Esperance Sportive de Tunis (Tunisia), Mamelodi Sundowns FC (Afrika Kusini), Atletico Petroleos de Luanda (Angola), Simba SC (Tanzania), TP Mazembe (DR Congo), na Wydad AC (Morocco).


MECHI 14


Katika michuano hiyo msimu huu zitapigwa jumla ya mechi 14, ambapo zitaanza kwa mfumo wa mtoano, kisha timu zitakazoshinda kwa matokeo ya jumla zitatinga nusu fainali kisha fainali itakayopigwa mara mbili. Ikumbukwe mechi zote kila hatua zitachezwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini.


JUMANNE NI CAIRO


Simba itaanza leo na Al Ahly nyumbani, kisha mechi ya marudiano itapigwa Cairo, Misri Oktoba 24, mwaka huu na mshindi wa jumla atatinga nusu fainali atakapokutana na mshindi kati ya Mamelodi na Atletico Petroleos de Luanda.


Mechi nyingine katika hatua hii ya kwanza ni Enyimba dhidi ya Wydad na TP Mazembe dhidi ya Esparence zote zikipangwa kupigwa Oktoba 22, huku ile ya Mazembe ikipangwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.


Timu nne zitakazoshinda kwa matokeo ya jumla zitatinga nusu fainali huku nne zilizoshindwa zikiaga mashindano.


Nusu fainali hizo mbili zinatarajiwa kupigwa pia kwa muundo wa nyumbani na ugenini, kati ya Novemba Mosi, hadi Novemba 5, mwaka huu na washindi watakutana Fainali ambayo nayo itapigwa nyumbani na ugenini, kuanzia Novemba 5, kisha marudio, Novemba 11 na Bingwa wa kwanza wa mashindano hayo atapatikana hapo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad