Uongozi wa Yanga umetoa kauli yake mara baada ya timu yao kupoteza mechi ya kwanza ya ligi ukisema wamepoteza mechi na sio ubingwa wao wanaoushikilia.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji akisema hatua ya timu yao kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu FC si kitu kipya, ingawa hawakutarajia matokeo hayo.
Arafat alisema hata msimu uliopita walipoteza mbele ya Ihefu FC kwenye uwanja huo huo, lakini bado wakatwaa ubingwa na pia wakacheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa baada ya matokeo hayo uongozi wao umeyachukua kama changamoto na sasa wanajipanga kuinuka na gia kubwa kurudi kwenye ramani ya ushindi kupitia mchezo wao ujao dhidi ya Geita Gold.
Yanga itakutana na Geita Gold, Jumamosi, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, mabingwa hao wakicheza mechi ya pili ugenini msimu huu.
“Hayakuwa matokeo ambayo tuliyatarajia lakini kuna wakati kwenye soka unatakiwa kupokea hali hiii, tumepoteza mchezo wa kwanza msimu huu, haina maana kwamba tumepoteza ligi nzima.
“Tunarudi kujipanga, mashabiki wetu wasitoke mchezoni kwa matokeo haya, jambo zuri yamekuja mapema, yanatupa nafasi ya kujipanga ndani na nje ya uwanja ili mchezo ujao turudi kwenye njia ya ushindi kama kawaida yetu,” alisema Arafat.