Utata Waziri Silaa Kuzuia Ujenzi Kituo cha Mafuta
Ikiwa siku mbili zimepita tangu Waziri wa Ardhi, Jerry Silaa aagize kusitishwa ujenzi wa kituo cha mafuta cha mfanyabiashara Ibrahim Shayo, utata umetanda kutokana na nyaraka kuonyesha ujenzi umefuata taratibu zinazotakiwa na mamlaka husika.
Juzi Silaa aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Moshi, kusimamishwa ujenzi wa kituo hicho katika eneo la Shabaha, kata ya Mawenzi, hadi Wizara itakapotoa uamuzi mwingine bila kutoa ufafanuzi wa kina wala kutoa nafasi kwa mmiliki kutoa ufafanuzi, licha ya kuwa na vibali halali.
Silaa alitoa agizo hilo akisema eneo hilo liko chini ya mita 200 kutoka kilipo kituo kingine cha mafuta cha Puma, jambo alilosema ni la hatari.
"Uongozi wa Manispaa, simamisheni ujenzi huu nitatoa maelekezo baadaye, kwani mlitengeneza sheria ambazo zitakuja kuleta matatizo hapo baadaye, kabla sijatoka Moshi nione hiyo stop oder," aliagiza Waziri Silaa.
Hata hivyo, agizo hilo la Silaa limekuja wakati mmiliki akiwa na vibali vyote muhimu vinavyotakiwa kutoka kwa taasisi na mamlaka husika.
Akizungumza na Mwananchi, Shayo alisema mradi wake umesitishwa ukiwa umefikia asilimia 60 ya ujenzi, akiwa ameshawekeza zaidi ya Sh400 milioni katika mradi huo wenye thamani ya jumla ya takriban Sh1 bilioni.
Alisema kabla ya kuanza uendelezaji alitafuta na kupata vibali vyote vinavyotakiwa kwa uwekezaji wa aina hiyo, mchakato uliochukua miezi tisa.
“Mimi si mgeni katika biashara hii, nazijua taratibu zote za kufuata kabla ya kuwekeza, nilitimiza matakwa yote ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwa na hati ya eneo yenye jina la kituo na mchoro, niliwasilisha halmashauri na wakanipa kibali Aprili 27, 2023,” alisema Shayo, ambaye awali hakuwa akitaka kuzungumzia sakata hilo kwa undani.
Alisema baada ya vibali hivyo viwili alitafuta cha Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) ambacho alipewa Juni 22, 2023 kikiwa na saini ya Waziri mwenye dhamana ya mazingira, kisha akaomba na kupata kibali cha Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).
Shayo alisema mahali anapojenga kituo hicho si karibu na kituo kingine kama inavyoelezwa, kwani wapo katika mitaa miwili tofauti.
Alisema wakati ujenzi ukisitishwa na waziri, alikuwa eneo la tukio lakini alipoomba kuelezwa sababu za kina za kuzuia aliambiwa amtafute kwa wakati wake.
Shayo anadai alifanya jitihada mbalimbali, lakini hakufanikiwa mpaka Waziri Silaa alipoondoka wilayani hapo.
Anadai aliwasiliana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Rashid Gembe ili kujua hatima ya mradi wake ambaye alimwambia hayo ni maelekezo kwake na yeye hana mamlaka ya kupindisha au kukataa maelekezo ya Waziri.
Gembe alipotafutwa na Mwananchi jana hakupatikana, lakini iliiona barua yake ya Oktoba 05, 2023 kwenda kwa Shayo ikimuelekeza kusimamisha ujenzi hadi atakapotaarifiwa kwa maandishi.
“Tarehe 27/04/2023 nilikupa kibali cha ujenzi namba 000062 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mafuta, rejea ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika eneo la ujenzi tarehe 05/10/2023 na maelekezo yaliyotolewa.”
Masharti ya leseni
Kwa mujibu wa Ewura, ili kupewa leseni ya kuuza mafuta ni sharti uwe na nakala ya nyaraka za usajili wa kampuni au leseni ya biashara, nakala ya hati miliki ya kiwanja palipojengwa kituo cha mafuta au uthibitisho kutoka mamlaka husika iliyoruhusu ujenzi wa kituo hicho na nakala ya kibali cha ujenzi kutoka Halmashauri au Manispaa husika.
Vilevile Ewura wanataka uwe na nakala ya cheti cha tathmini ya athari ya mazingira kinachotolewa na Nemc, nakala ya cheti cha mlipakodi, nakala ya cheti cha zimamoto kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, kibali cha ujenzi kutoka Ewura (kwa vituo vilivyojengwa baada ya Aprili 2009) na orodha ya miundombinu iliyopo.