Vilio tu! Moto Ulivyoteketeza Mali za Wafanyabiashara Kariakoo

Vilio tu! Moto Ulivyoteketeza Mali za Wafanyabiashara Kariakoo


Matukio ya moto jijini Dar es Salaam yameendelea kuleta hasara, huzuni na vilio, safari hii yakiteketeza maduka, majengo na migahawa iliyopo Kariakoo.


Moto huo ambao chanzo chake bado hakijafahamika ulianza saa 12 asubuhi katika eneo la Mnadani kunakouzwa vifaa vya magari na baada ya kuzuka ulisambaa katika majengo mengine likiwemo la Big Bon ambalo ndani yake kuna benki ya BoA.


Katika eneo la tukio, imeshuhudiwa baadhi ya wananchi wakibubujikwa na machozi kwa huzuni kutokana na kuungua moto kwa bidhaa zao.


Ilikuwa ni mwendo wa kupigiana simu kwa wananchi wa maeneo mbalimbali kujulishana kuhusu uwepo wa moto ambao kadri muda ulivyozidi kwenda ulikuwa ukisambaa katika maeneo mengine.


Ni watu wachache waliofanikiwa kuokoa mali zao kwa sababu wengi wao hawakufungua maduka, hata walipopata taarifa walikuta moto umeshaziteketeza.


Lakini wengine walifanikiwa kutoa mali zao huku wakipata hasara kwani hawakufanikiwa kuziokoa zote.


Kilichoshuhudiwa ni pilika za huku na kule kila mmoja akijaribu kila linalowezekana kuhakikisha anaokoa mali zake.


Ulivyoiona Big Bon eneo la Msimbazi jana ni tofauti na lilivyo leo, kwani moto huo umeathiri hadi taswira ya eneo hilo.


Pamoja na wananchi, jeshi la Polisi pia lilishuhudia likiimarisha ulinzi katika eneo hilo ambalo ndilo kitovu cha biashara katika Jiji la Dar es Salaam.


Moto huo umesababisha barabara ya Mtaa wa Msimbazi kufungwa kwa zaidi ya saa tatu tangu asubuhi baada ya tukio hilo kutokea.Kwa watumiaji wa barabara hiyo wanalazimika kutumia njia mbadala ikiwemo mabasi yaendayo haraka.


Mmoja wa mashuhuda ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini amesema moto huo umeanzia katika majengo yaliyopo mitaa Mafia na Mkunguni.


Amesema moto huo umeanzia eneo la mnada ambako kunahifadhiwa vitu vilivyotumika ikiwepo mitungi ya gesi umesababisha hasara kwa wafanyabiashara ambao baadhi yao hawakubahatika kutoa vitu vyao.


Kwa mujibu wa shuhuda huyo ambaye ni mfanyabiashara ametoa vitu vyake nje ya moja ya jengo lililokuwa linaungua baada ya kupigiwa simu na mtu ambaye hamfahamu na kumtaka aende dukani kuna moto.


"Nimechanganyikiwa kutokana na hali hii sijui hata cha kuongea ninachoshukuru nimeokoa baadhi ya viti tu," amesema.


Mmoja wa mfanyakazi wa BoA ambaye hakutaja jina lake amesema taarifa za moto alizipata asubuhi kutoka kwa mlinzi aliyekuwa zamu.


"Tumetoa baadhi ya vifaa ambavyo vilikuwa karibu vingine tumeacha kutokana na ongezeko la moto,"amesema mtu huyo.


Mnadani ni eneo la ambalo linauzwa spea za magari yaliyotumika, mikanda ya kufungia magari makubwa ya kubeba mizigo ambapo kuna vibanda takribani 50


Mkazi wa Kariakoo, Mohamed Haron amesema moto huo ulianza saa 12 asubuhi kwenye moja ya duka linalouza spea za magari na pikipiki na baadaye kusambaa kutokana na upepo uliokuwa na kasi kubwa.


Haron amedai kutokana jeshi la zimamoto na uaokoji kuchelewa eneo la tukio moto ulianza kusambaa kwa kasi kwenye maduka ya jirani kisha kupanda ghorofani.


Shuhuda mwingine Jasmin Anuary naye ameitupia lawama zimamoto huku akisema miundombinu ya kupambana na majanga siyo rafiki ndio maana moto huo ulisambaa kwa kasi.


Amesema kuuwa hata gari la Zimamoto liloilofika limekuwa likipambana na moto wa chini huku moto wa juu ukiwa ni changamoto kuuzima kutokana na vifaa kutokuwa na uwezo.


Baadhi ya viongozi wakuu wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Dar es Salaam, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila wamewasili Kariakoo na kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali yalioungua

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad