Waamuzi wawili mechi za Simba ugenini wasimamishwa, Kamwe kimemkuta0




Mwamuzi msaidizi namba mbili wa mechi ya Tanzania Prisons vs Simba ya Ligi Kuu iliyochezwa ugenini mkoani Mbeya, Nestory Livangala na mwamuzi msaidizi namba mbili Abdallah Bakenga wa Kigoma aliyekuwa katika mechi ya Singida Big Stars vs Simba ikipigwa Singida wameondolewa kwenye ratiba ya waamuzi kwa mizunguko mitano kila mmoja kwa kosa la kushindwa kutafsiri vyema sheria za mpira wa miguu.

Katika mechi hizo Simba ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Prisons na 2-1 dhidi ya Singida Big Stars.

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu imetoa maamuzi hayo leo ambapo pia Singida BS imetozwa faini Sh1 milioni kwa kosa la wachezaji wake kuingia uwanjani kupitia mlango usio rasmi.

Waamuzi wengine waliosimamishwa mechi tano ni Walter Josephat, Misango Parapara katika mechi ya Dodoma Jiji na Azam FC iliyomalizika 0-0 na mwamuzi Florentina Zabron katika mechi ya Mtibwa na Singida Big Stars uliomalizika kwa Singida BS kushinda 1-0.


Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe ametozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kumkejeli na kumdhalilisha mwamuzi wa mechi ya Singida Big Stars dhidi ya Simba kupitia mtandao wa kijamii.

"Baada ya kumalizika kwa mechi, Ali Kamwe aliweka chapisho katika ukurasa wake binafsi wa mtandao wa kijamii wa Instagram, ambalo lilikuwa na picha ya mwamuzi (Malogo) huku akiunganisha na wimbo ww msanii wa muziki kizazi kipya, Billnass uitwao Maokoto, hali iliyoleta tafsiri ya kumhusisha mwamuzi huyo na masuala ya fedha ama rushwa," imeeleza taarifa ya Bodi ya Ligi.

Pia, klabu ya Yanga imetozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la mashabiki wake kurusha chupa za maji kiwanjani baada ya timu ya Ihefu kufunga bao la pili.

Katika mechi hiyo iliyopigwa uwanja wa Highland Estate mkoani Mbeya, Ihefu ilishinda mabao 2-1.

Yanga pia imetozwa Sh1 milioni kwa kosa la maofisa wa benchi la ufundi kuonekana wakipinga maamuzi ya waamuzi wa mchezo huo na kumzonga mwamuzi wa akiba.

Makosa hayo yameainishwa katika taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu iliyotolewa leo Oktoba 19 baada ya kikao cha maamuzi kuketi jana

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad