Waathirika wa moto Kariakoo wazua vurugu





Dar es Salaam. Wafanyabiashara  waliounguliwa maduka na vibanda katika eneo la Mnadani, Kariakoo wamezua vurugu zilizosababisha kuvunja geti.

Awali, wafanyabiashara hao walikusanyika katika eneo hilo ambalo kwa sasa linalindwa na walinzi.

Wakiwa hapo, baadhi waliwashinikiza walinzi kufungua geti lililotengenezwa kwa mabati na walipokataa kufanya hivyo, walilisukuma na kuingia ndani.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Oktoba 12, 2023, Hamis Mikidadi amesema tangu walipoelezwa kwamba tume inaundwa kuchunguza tukio la moto kumekuwa na ukimya.


Mikidadi amesema hawajui kinachoendelea, huku wao ‘wakifa njaa’ kwa kuwa eneo hilo ndipo walipokuwa wakipategemea kupata riziki.

Kwa upande wake, Said Salim amesema wakati wao wakizuiwa kuingia eneo hilo, waathirika wengine wa tukio la moto wanaendelea na shughuli zao ikiwamo kukarabati majengo.

"Kama kusubiri tume wote tungesubiri, si wengine wanakarabati maeneo yao, sisi tunazuiwa tusiingie wakati hii ni sehemu yetu ya kazi," amesema Salim.


Moto katika eneo hilo ulizuka Oktoba mosi, 2023 na kuteketeza bidhaa zilizokuwamo kwenye maduka na vibanda vinavyotumika kuuzia vipuri vya magari na mitambo vilivyotumika pamoja na vyuma chakavu.

Mwananchi Digital, ilipomtafuta Mkuu wa Wilaya ya Ilala, simu yake iliita bila kupokelewa lakini bado jitihada za kuitafuta mamlaka husika inaendelea, endelea kufuatilia mitandao yetu kwa taarifa zaidi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad