Tel Aviv. Idadi ya waliokufa pande zote mbili zinazopigana kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas la nchini Palestina imefikia zaidi ya watu 1,100 hadi sasa huku maelfu wakijeruhiwa.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema leo Jumatatu Oktoba 9, 2023 kuwa takriban watu 700 wameripotiwa kuuawa huku watu wengine 1,200 wamejeruhiwa wengi wao wakiwa mahututi kadhalika kwa upande wa Palestina idadi ikifikia zaidi ya watu 400.
Idadi hiyo imekuja ikiwa imeingia siku ya tatu ya mapigano ambayo yalizuka rasmi alfajiri ya Jumamosi ambapo Hamas walifanya shambulio la kushtukiza nchini Israel kwa kurusha rundo la makombora.
Saa chache baadaye Israel ilijibu mashambulizi ya angani na ardhini huko ukanda wa Gaza ambapo wanamgambo wa Hamas wanatajwa kujipenyeza na kuingia upande wa Israel ambapo wametekeleza mauaji ya watu pamoja na kuwateka nyara.
Msemaji wa ID, Luteni Kanali Jonathan Conricus amenukuliwa na AFP kuwa karibu wanamgambo 1,000 wa Kipalestina walishiriki katika shambulio la Hamas ambalo aliliita ‘siku mbaya zaidi katika historia ya Israeli’.
Takriban wanajeshi 100,000 wa akiba wametumwa kusini wakati IDF ikipambana kuwafukuza wapiganaji wa Hamas kutoka eneo la Israel, amesema na akiongeza kuwa watu wengi pamoja na wanajeshi wa Israel wanazuiliwa ndani ya Gaza.
"Ndege za kivita za IDF, helikopta, na makombora zimeshambulia zaidi ya maeneo 500 ya magaidi wa Hamas katika Ukanda wa Gaza," jeshi limesema katika taarifa ikieleza mashambulizi yaliyofanyika usiku kucha.