Wasicha Mapacha Wafariki kwa Kupaka Dawa Kuongeza Ukubwa wa Matiti Bariadi
Watoto wawili mapacha (17), wamefariki dunia huku chanzo kikitajwa kuwa ni dawa za asili walizopewa na mganga wa tiba hizo kwa lengo la kuongeza matiti ili waweze kuolewa.
Marehemu hao walikuwa wakazi wa Kijiji cha Lubale, Kata ya Nkororo, Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, ambapo imeelezwa kuwa mganga anayetuhumiwa kufanya kitendo hicho Masunga Tumoro, akiwa ametoroka na juhudi za kumsaka zinaendelea.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Simon Simalenga aliyefika eneo la tukio, amelaani kitendo cha mganga huyo kutoa dawa hizo na kuliagiza jeshi la polisi wilayani humo kumsaka mtuhumiwa ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
"Mganga apatikane awe amekimbia au amekwenda wapi na kama mmemkamata mke wake akae ndani hadi huyo mwanaume ambaye ni mganga apatikane," amesema Simalenga.
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Biunada, Dk Deogratius Mtaki, amesema kuwa tukio hilo limetokea alfajiri ya kuamkia jana Oktoba 4, 2023; na kwamba wakati Kulwa Yohana amepokelewa saa 10 alfajiri akiwa amekwisha fariki, Dotto Yohana yeye alipokelewa saa 12 asubuhi akiwa mahututi na kwamba saa tatu baada ya matibabu, alifariki.
Akizungumzia tukio hilo baba mdogo wa marehemu hao Daniel Mishael amesema dawa waliyopewa ilikuwa ya kupaka na baada ya siku mbili hali ikabadilika.
"Hata hivyo, kutokana na maelezo ya daktari, amesema dawa zilizotumika zilikuwa nyingi sana na ambazo zilibadilika na kuwa sumu mwilini kwani amesema ziliingia kwenye maini na pia ziliwasababisha watapike damu na kuharisha," amesema Mishael.
Kwa upande wake jirani wa mtuhumumiwa, Lucia Kadilo amesema waganga hawatakiwi kuingilia mipango ya Mungu katika uumbaji. "Mungu ndiye anayemuumba binadamu na kumpa viungo vyote," amesema.
Jirani huyo anaamini kuwa hiyo ni kesi ya mauji kama zilivyo kesi nyingine na kwamba mtuhumiwa anatakiwa kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.