Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema hana taarifa yoyote kutoka kwa mabosi wa klabu hiyo kuhusiana na yeye kukalia kuti kavu katika nafasi yake anayoitumikia.
Baada ya Simba SC kupoteza mechi dhidi ya Young Africans, kulikuwa na tetesi za ofisa huyo kusimamishwa pamoja na wachezaji watano huku tayari Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amefukuzwa kazi.
Ahmed amesema yeye anaendelea vyema na majukumu yake lakini kama viongozi wake wataona kuna haja ya kufanya maboresho katika nafasi yake kwa manufaa ya Simba SC yupo tayari.
“Sina taarifa kutaka kuondolewa kwenye nafasi yangu, naendelea na majukumu yangu kama kawaida, lakini kama uongozi utakuwa na jambo lolote nitapewa taarifa na nitakubaliana na kile nitakachoelezwa,” amesema Ahmed.
Ameongeza mechi dhidi ya Young Africans imeshapita na sasa wanaelekeza akili na nguvu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC utakaochezwa leo Alhamis (Novemba 09) na kikubwa wamejipanga kusahihisha makosa ili kurejesha morali ya wachezaji wao.