Baada ya Simba SC kuchezea kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Young Africans, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla amewataka Mashabiki na Wanachama wa Simba SC wasahau matokeo hayo kwani hayajabadili chochote kwenye historia ya vipigo baina ya timu hizo.
Makalla ambaye ni shabiki wa Simba SC ameyasema hayo akifafanua kufungwa huko hakujapindua historia yoyote ya vipigo walivyowahi kuichapa Young Africans, ikiwemo 5-0 na 6-0 hivyo wasiwe na wasiwasi na waendelee na kazi kama kawaida bila ya mawazo yoyote.
“Mimi niwashauri kuwa habari za jumapili za kufungwa wazisahau waendelee kuchapa kazi kama kawaida, sababu matokeo hayo hayajapindua historia yoyote maana Young Africans ilishafungwa mabao 6-0, mabao 5-0, kwa hiyo wala wasipate tabu, iko hivyo,” amesema Makalla.
Kiongozi huyo amekumbushia vipigo hivyo vilivyotokea mwaka 1977 ambapo Simba SC ilishinda kwa mabao 6-0 huku mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni akifunga mabao matatu, kipigo kingine ni cha mwaka 2012, ambapo Simba SC ilishinda mabao 5-0.
Hata hivyo, Mashabiki na Wanachama wa Young Africans wamekuwa wakitamba kulipiza kisasi baada ya ushindi wao huo wa juzi Jumapili (Novemba 05) wa mabao 5-1 uliopatikana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.