TABU iko palepale! Ndivyo unavyoweza kusema, kwani kuna uwezekano mkubwa balaa la Stephane Aziz Ki likaendelea kuzitesa timu nyingi Bongo, ambapo imefichuka uongozi wa Yanga unamuandalia mkataba wa mnono staa huyo.
Aziz Ki ambaye alijiunga na Yanga kupitia dirisha kubwa la usajili msimu wa 2022/23 na kusaini mkataba wa miaka miwili, anatarajiwa kumaliza mkataba huo mwishoni mwa msimu huu.
Chanzo kutoka ndani ya Yanga, kimeliambia Spoti Xtra, kuwa mabosi wa timu hiyo wameanza mchakato wa kumpa mkataba mpya staa huyo mapema ili kuepuka uwezekano wa kumpoteza bure mwisho wa msimu.
“Kwa uwezo ambao anauonesha Aziz msimu huu, ni wazi litakuwa jambo la ajabu kuona tunampoteza bure mwishoni mwa msimu, hivyo uongozi umeanza haraka mchakato wa mazungumzo ya awali ya kumpa mkataba mpya ambao unatarajiwa kuwa na thamani kubwa kuliko ule ambao alisaini wakati anakuja. Tunafahamu kuna baadhi ya timu kubwa nazo zimeanza kumfuatilia,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumzia suala la uboreshaji wa mikataba ya wachezaji wa timu hiyo, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, alisema: “Suala lolote la mikataba linategemea na mahitaji ya kocha, hivyo tutahakikisha tunatimiza matakwa ya kumbakisha mchezaji yeyote na kuongeza nguvu kwa kuleta mastaa wapya pale inapohitajika.”
Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya timu hiyo, Rodgers Gumbo, alisema: “Malengo yetu ni kuhakikisha tunakuwa na timu ambayo itaandika historia katika mashindano ya kimataifa, hivyo tuko tayari kulipa gharama yoyote kufanikisha hilo.”