Mchambuzi wa masuala ya soka nchini kupitia Clouds FM na shabiki wa Klabu ya Simba, Farhan Kihamu amehoji uwepo wa (utambulisho wa biashara) logo mbili za Mo Xtra kwenye jezi mpya walizozindua Simba kuelekea michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kihamu amesema kuwa, viongozi wa Simba walipaswa kutafuta mdhamini mwingine kwa ajili ya kuweka kwenye jezi hizo ili kuwapa fursa wafanyabiashara wengine kujitangaza kupitia Simba na kuiongezea klabu mapato.
“Labda CEO atusaidie kidogo majibu ni kwamba hakuna Mdhamini mwingine wa kuweka hela ama? Mo Xtra zipo mara mbili, juu kulia na moja kubwa mbele kifuani, kabisa hakuna brand nyingine? Jezi moja ina matangazo mawili ya kufanana?
“Tajiri anatoa mzigo yes lakini hii ya kutuweka matangazo ya kufanana kwenye uzi mmoja ni kubana fursa nyingine za klabu kuingiza pesa ya kutosha kutokana na platform hii kubwa ya michuano ya kimataifa.
“Halafu CEO pia atusaidie hiyo Mo Sport mkataba wake ulisainiwa lini? Ni Kampuni ya nani hii? Inajihusisha na nini hii? Ni hayo tu kwasasa, ni hayo tu,” amesema Farhan.