Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ametoa siku tano kwa wamiliki wa madanguro akiwataka kuyavunja wenyewe, na kwamba wasipofanya hivyo, atataifisha nyumba hizo.
Pia amewaagiza wamiliki wa baa zote ambazo nje kunafanyika biashara hiyo kuhakikisha wanawaondoa vinginevyo atazifunga.
Chalamila ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Novemba 3, 2023 wakati alipotembelea madanguro yaliyovunjwa na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni.
Novemba Mosi mwaka huu Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge akishirikiana na Mkuu wa Wilaya hiyo Saad Mtambule, walivunja madanguro hayo na kuwakamata baadhi ya wasichama waliodaiwa kuhusika kufanya biashara hiyo.
Chalamila amesema, nyumba zilizopewa leseni kwa ajili ya makazi na kubadilishwa matumizi ni kosa kisheria na kuwataka kuzivunja ndani ya siku tano.
"Nitoke siku tano nyumba zote zilizojengwa na kugeuzwa madanguro muwe mmezivunja vinginevyo ntazitaifisha,"
"Na wale wamiliki wa baa ambazo nje biashara hii inafanyika, wakina dada wanakipanga, ikome mara moja vinginevyo nitazifinga zote, hatuwezi kulea ujinga wa namna hii," amesema Chalamila.
Hata hivyo RC huyo Wakuu wa Wilaya katika mkoa huo kuhakikisha operesheni hiyo inaendelea kwenye maeneo yay a kiutawala na kwamba wahakikishe biashara hiyo inakomeshwa.
Kuhusu biashara ya kusingwa mwili (massage) amesema baadhi ya saluni zinatoa huduma hiyo.
Alisema siku chache zilizopita kuna mtu alifariki kwenye chumba akipatiwa huduma hiyo, na kwamba ni ngumu kujua ni nini kilichompata na kuwataka viongozi hao kuzichunguza.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule alisema eneo hilo lina nyumba nane zenye leseni za makazi lakini zimegeuzwa kuwa madanguro.
Alisema Juni mwaka huu walifanya kikao na wamiliki wa nyumba hizo pamoja na viongozi wa dini, nakukubaliana kuzibomoa lakini wakaomba kupewa miezi sita ili waweze kuondoka, japo walikuta biashara hiyo ikiendelea.
Amesema baada ya kujuta biashara hiyo inaendelea, waliamua kuchukua hatua ikiwemo kung'oa milango nakuwataka wamiliki wa nyumba hizo kuzivunja wenyewe kabla hawajachukua hatua zaidi.
"Tutaendelea kuchukua hatua kama ulivyotuelekeza, wakina dada hao wanazo kazi nyingi ambazo wangeweza kuzifanya ikiwemo kukopa mikopo ya asilimia kumi na kufanya biashara," alisema.
"Tumeendelea kushirikiana na baadhi ya kina dada ikiwemo watatu waliokuwa wakifanya biashara eneo hili wapo tuliowashauri, wakachukua ushauri wetu lakini wengi walimekaidi," amesema Mtambule.
Amebainisha kuwa wote wenye madanguro wanafahamika kwa muda mrefu na kwamba hatua hiyo ya utekelezaji ilikuwa ni suala la muda tu, hivyo wataaamia na maeneo mengine.
Kwa upande wake Meya wa Kinondoni Songoro Mnyonge amesema wamedhamiria kukomesha biashara hiyo ilivyokuwa inadhalikisha utu wa mwanamke kwa muda mrefu.
Amesema watu waliokuwa hapo wameamua kukaa kimya na kusababisha watoto wadogo kufanya vitendo visivyo na maadili wakiwemo wanafunzi.
"Chakusikitisha biashara hiyo inaanzia Sh1, 000 hadi 3,000, pale Halmashauri kuna mikopo ya asilimia kumi timewaambia waje wakope waachane na hii biashara wengi wao hawataki," amesema.