Hatima ya Chongolo CCM kujulikana leo




Dar es Salaam. Barua inayodaiwa kuandikwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, kuhusu kujiuzulu wadhifa huo, ni miongoni mwa mambo yanayojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho leo.

Katika kikao hicho kinachofanyika Ikulu ya Dar es Salaam, Chongolo ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria kulingana na chanzo cha kuaminika ndani ya chama hicho.

Kama itathibitika mwanasiasa huyu ameandika barua hiyo, atakuwa amedumu kwenye wadhifa huo kwa siku 942, kwani alichaguliwa na Halimashauri Kuu (NEC) ya CCM Aprili 30, 2021 akirithi mikoba ya mtangulizi wake Dk Bashiru Ally ambaye hivi sasa ni mbunge wa kuteuliwa. 

Vuguvugu la kung’atuka kwa Chongolo katika nafasi hiyo, liliibuka kupitia barua inayodaiwa kuwa ameiandika Novemba 27 mwaka huu, kwenda kwa Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan ambayo imesambaa katika mitandao ya kijamii.

Barua hiyo inaeleza sababu za kung’atuka katika nafasi hiyo kuwa ni “kuchafuliwa katika mitandao ya kijamii,” huku msingi mkuu wa uamuzi huo kwa mujibu wa barua hiyo ni “kuwajibika kama kiongozi kwa masilahi ya chama” wakati wote anapotuhumiwa au kuhusishwa na jambo lolote.

Leo Jumatano, Novemba 29, 2023; Mwananchi Digital imedokezwa juu ya suala la barua hiyo kuwa sehemu ya mambo yatakayojadiliwa katika kikao hicho cha maamuzi.

Kwa mujibu wa chanzo hicho kilichoomba hifadhi ya jina lake, uhakika wa barua hiyo kama imetoka kwa Mtendaji Mkuu huyo wa CCM, utajulikana kwa kuwa ni moja ya mambo yaliyowekwa mezani kuzungumzwa.


“Hilo halina jibu bado (kuhusu kama ni barua ya Chongolo au la), lakini limeletwa kwenye vikao na leo tutaendelea na NEC Ikulu Dar,” kimeeleza chanzo hicho.

Kilipoulizwa iwapo Chongolo ni miongoni mwa wajumbe waliohudhuria kikao hicho, chanzo hicho kilikiri uwepo wa kiongozi huyo katika ukumbi wa kikao leo.

Madai ya kujiuzulu kwake yalipata mashiko zaidi jana, hasa pale ambapo hata picha zilizosambazwa za kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Chongolo hakuonekana kama inavyotakiwa kwa kuwa yeye ndiye mtendaji mkuu.

Jambo hilo, liliongeza hisia kwamba Katibu Mkuu huyo hakuwepo hata katika semina iliyoandaliwa kwa ajili ya wajumbe wa NEC iliyofanyika jana Ikulu.

Liya ya kuwapo kwa taarifa za kutatanisha juu ya kujiuzulu kwa mwanasiasa huyo, si yeye wala chama kilichojitokeza kueleza ukweli wa jambo hilo.

Hata hivyo, kwa maelezo ya chanzo hicho, ukweli wa barua hiyo na hatma ya wadhifa wa Chongolo utajulikana katika leo wakati wa vikao vya CC na NEC.

Utaratibu wa kiongozi kujiuzulu ndani ya CCM umeelezwa katika katiba ya chama hicho ibara ya 130 (1), inayoeleza kiongozi anayetaka kung’atuka atafanya hivyo kwa kuandika barua ya kung’atuka kwake na kuipeleka kwa Katibu wa kikao kilichomchagua au kumteua.

Namna nyingine kulingana na katiba hiyo ibara 130 (2), anayeng’atuka atatangaza uamuzi huo mbele ya kikao kilichomchagua.


Hata hivyo, Kamati Kuu ndicho kikao kinachomthibitisha Katibu Mkuu wa CCM baada ya jina lake kuwasilishwa mbele ya wajumbe kutoka kwa Mwenyekiti na hivyo kikao cha leo ndicho kinachostahili kuarifiwa uamuzi wa Chongolo iwapo upo kama inavyoelezwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad