Imefichuka; Kisasi cha Damu Nacho Kimelipwa kwa Damu

 

Wanasema Waislamu. Kisasi ni haki. Miaka 11 iliyopita, Juma Kaseja alipiga penalti iliyoipatia Simba bao la tano katika ushindi wa kushangaza wa mabao matano wa Simba dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Taifa. Nchi nzima ilizizima. Yanga haikuwa na majibu jioni ile ambayo Emmanuel Okwi alitamba uwanja mzima na kufunga mabao mawili kati ya matano.


Miaka 11 baadaye, Yanga imefanya kilekile ambacho ilifanyiwa na Simba katika mahakama ileile. Temeke. Pacoume Zouazou akifunga bao la tano kwa mkwaju wa penalti baada ya Maxi Nzengeli kukatwa ngwala ya wazi na Henock Inonga ndani ya boksi. Ni katika mechi ambayo Nzengeli kama ilivyokuwa kwa Okwi naye aliondoka na mabao mawili katika nyavu za Aishi Manula.


Kisasi ni haki, lakini haikuonekana kama kungekuwa na kisasi katika jioni hii ambayo mchezo ulichezwa katika uwanja ulioloa, lakini ambao haukuwa na utelezi. Ni kufuatia mvua kali inayoliandama Jiji la Dar es salaam. Kisasi hakikuonekana kinakuja wakati Kennedy Musonda alipofunga bao la kuongoza dakika ya tatu ya mchezo kisha Kibu Dennis akasawazisha dakika sita baadaye.


Staili ilikuwa moja. Mabao ya vichwa. Hawa hapa mpira wa krosi, wale pale mpira wa kona. Wakati timu zinakwenda vyumbani Yanga waliuacha uwanja ukiwa umechangamka kidogo kuliko Simba. Kipindi cha pili walichangamka zaidi na kuiua Simba kiulaini kabisa.


Sababu ya kwanza ya Yanga kuiua Simba ilikuwa rahisi tu. Yanga ilikuwa bora wakati haina mpira. Timu zote bora duniani ni zile ambazo zinakuwa bora wakati hazina mpira. Miguel Gamond ameng’amua hili. Yanga ilikuwa bora wakati haina mpira. Walikuwa wanawahi mipira yote ya kwanza ambayo ilikuwa inazagaa au inagombaniwa.


Mabao yote ya Yanga yalitokana na hili jambo. Ama kuwahi mpira unaozagaa au kuwalazimisha Simba wawape mpira kwa kuwakaba kwa haraka. Mfano bao la kwanza Yao Kouassi aliuwahi mpira uliokuwa umeoshwa na beki wa Simba. Akaunasa akampiga chenga mchezaji mmoja wa Simba akatia krosi kwa Musonda akafunga.


Bao la pili, Clatous Chama alikuwa anampasia mshambuliaji wake wa kati lakini Ibrahim Bacca akautokea akasogea nao mbele ikatokea songombingo ndogo akaendelea kuwa nao akampasia Aziz Ki ambaye alikokota na kupiga pasi kwa Maxi Nzingeli aliyemfunga Manula kwa urahisi kabisa. Nadhani Aishi hakutazamia kwamba Maxi angefunga hapo hapo. Alijua angetuliza na kuuweka sawa mpira lakini alipiga hapo hapo kwa mguu wa kushoto.


Bao la tatu Yanga walipora tena mpira. Sadio Kanoute alijaribu kupiga pasi kwenda kwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, lakini Yao Yao Kouassi akautokea akaunasa akampasia Pacoume ambaye alimtoka Kanoute na kuukimbiza mpira mbele kwa Clement Mzize ambaye alimtoka mlinzi mmoja wa Simba na kumpasia Aziz Ki. Shomari Kapombe alikuja kukaba kwa nguvu akakwepwa Aziz akafunga. Linaweza kuwa bao lake la nne dhidi ya Aishi tangu akiwa Asec Mimosas.


Bao la nne, Yao Yao alikuwa amemkaba vema Osamba Onana huku pembeni. Pacoume akaupitia akampigia kisigino Yao Yao. Zikapigwa pasi nne za haraka haraka Aziz akampasia Mzize ambaye aliingia na nguvu nyingi zilizowachosha mabeki wa Simba. Tshabalala akajaribu kufukuza upepo hakuweza. Mzize akampasia kwa urahisi Nzingeli aliyefunga kwa urahisi tu kama vile walikuwa mazoezini.


Bao la tano lilikuja hivyo hivyo. Simba waliosha mpira ambao Joyce Lomalisa aliutokea hewani na kuurudisha kwa pasi safi kwa Aziz Ki ambaye aliuparaza kwa umaridadi mkubwa kwenda kwa Nzengeli ambaye alichomoka vema lakini akakatwa mtama na Inonga. Penalti. Pacoume akafunga.


Ambacho Yanga haikujua ni kwamba kama penalti ile angepewa Nzengeli halafu akafunga basi ingekuwa hat trick na angekuwa ameifikia rekodi ya miaka 46 iliyowekwa na staa wa zamani wa Simba, Abdalah ‘King’ Kibaden mwaka 1977 ya kuwa mchezaji pekee nchini aliyewahi kufunga hat trick pambano la Simba na Yanga.


Labda walitaka utatu wao mtakatifu uondoke uwanjani huku kila mmoja akiwa amefunga. Namaanisha Nzengeli, Aziz pamoja na Pacoume. Acha Kibaden aendelee kujidai na hat trick yake ambayo ina umri wangu. Hawa wakubwa wanafanya uzembe wa makusudi kudumisha rekodi yake.


Simba nayo iliwahi kuupuzia jambo hili. Siku ile ambayo waliibamiza Yanga mabao matano walipata penalti. Badala ya kumpatia Okwi afunge hat trick wao wakaamua kumpatia Kaseja. Ni katika siku njema kama ile nadhani na wao walitaka hadi kipa wao afunge bao. Na kama Mwamuzi Ahmed Aragija angekuwa makini zaidi basi huenda Yanga ingelipa kisasi cha 6-1 ilichopokea siku hiyohiyo ambayo Kibadeni alipiga hat trick. Ilikuaje hakuona wakati Kapombe alipoukumbatia mguu wa Mudathir Yahaya katika boksi la Simba? Ilikuwa penalti ya wazi.


Tukiachana na namna ambavyo Yanga ilionekana kupora mipira kwa urahisi kuliko Simba, Yanga pia ilionekana kuwa na haraka ya kuwahisha mpira mbele. Wazungu wanaita ‘transition’. Walipopora tu waliupeleka mpira mbele kwa kasi. Na kwa sababu walikuwa wamepora mara nyingi waliwakuta Simba wakiwa hawajajipanga. Kasi yao iliwachanganya mabeki wa Simba na kujikuta wakikatika.


Yote haya mawili yanatokana na nini? Mambo mawili. Kwanza kabisa achilia mbali uwezo wa mchezaji mmoja mmoja lakini Yanga ina utimamu mkubwa wa mwili. Juzi walikuwa wanacheza wakiendelea kukifanya kile kile walichokifanya Tanga wakati timu hizo zilipokutana mara ya mwisho. Simba aliondoka na matokeo ya penalti lakini Yanga iliikamata mechi kwa dakika 90.


Kitu kingine ambacho kiliisaidia Yanga ni Simba kukosa heshima kwao. Kama Robertinho angekuwa ameifuatilia vema Yanga basi angecheza kwa nidhamu na kuwanyima nafasi. Hata hivyo, alicheza kama vile anacheza mechi nyingine tu. Labda kwa sababu alishinda katika pambano la pili raundi iliyopita. Au labda kwa sababu alipata ushindi wa penalti Tanga.


Kwa sasa Yanga ni bora kuliko Simba. Timu zote ambazo hazikuwaheshimu Yanga msimu huu zilibondwa vibaya. Huu sio ushindi wa kwanza wa mabao matano wa Yanga msimu huu. Timu ambayo ilicheza na Yanga vema zaidi ilikuwa ni JKT Tanzania ambayo ilifungwa bao la jioni na Mudathir Yahaya pale Mbagala katika Uwanja wa Mzee Bakhresa. Simba walipaswa kuwa makini zaidi.


Lakini pia tusisahau kwamba lilikuwa suala la muda kabla ya Simba kupokea kichapo hiki. Sio kwa Yanga, bali kwa timu yoyote yenye uwezo. Ingeweza kufungwa mabao haya katika kipindi cha kwanza tu cha pambano dhidi ya Al Ahly nyumbani. Ni wenyewe tu Al Ahly walipoteza nafasi hovyo. Simba ilikatika hovyo katika kipindi cha kwanza. Kule Cairo ndio ilikwenda kucheza vizuri.


Lakini kabla ya hapo Simba haikuwa inacheza vema. Baadaye tukasikia kwamba ili mradi pointi tatu zinapatikana basi hilo lilikuwa jambo la msingi kuliko kucheza vizuri. Ilitushangaza sisi wengine kwa sababu utamaduni wa Simba ni kuweka mpira chini na ndio kuna wakati miaka ya 1980 walikuwa wanaitwa Lunyasi. Waliuweka mpira katika nyasi na ukatulia hasa.


Kuna kelele zimepigwa kuhusu Manula. Nadhani kwa sababu amefungwa mabao matano huku ikiwa ni mechi yake ya kwanza akirudi katika lango la Simba watu wamekariri kwamba Ally Salim angefanya vema zaidi. Siamini katika hili. Ni kweli ulikuwa mtego kumrudisha Aishi moja kwa moja katika mechi ngumu lakini sidhani kama kuna bao lolote unaloweza kusema ni kosa lake la moja kwa moja.


Katika kuanzisha mipira na kupiga pasi Aishi hayupo vizuri na wote tunafahamu lakini katika kuruhusu mabao sijaona makosa yake. Kama kuna bao lolote angeligeuza kuwa mchomo basi tungeweza kupiga makofi na kusema amefanya kitu kisicho cha kawaida. Lakini kama amefungwa bado hauwezi kusema amefanya uzembe.


Robertinho? Tusubiri na kuona hatima yake itakuwa vipi. Mpaka wakati huu naandika sina uhakika sana kama Simba itakwenda naye katika mechi za makundi. Sina uhakika. Nazijua timu zetu. Kipigo cha mabao matano huwa kinakuwa na maana kubwa kwao. Hakimuachi mtu salama. Kama atabakia basi timu inabidi iimarike sana. Simba haipo fiti.


Ukiachana na jambo hilo Simba pia ijitafakari. Inaendelea kukosea katika usajili kiasi kwamba wachezaji wake wanakuwa wale wale tu. Leo Robertinho anadai timu haikushinda kwa sababu Kibu Dennis alipata majeraha. Vipi kwa Yanga ambayo imemuuza Fiston Mayele kisha ikawaondoa kina Djuma Shaban na Yannick Bangala?


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad