Dar es Salaam. Baada ya kimya kirefu hatimaye, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ameibuka tena na kudai uhakiki wa nyaraka ikiwemo uraia ni moja ya mambo yanayochelewesha ofisi yake kutoa usajili wa muda kwa vyama 18 vilivyoomba.
Hiyo ni sababu ya pili kutolewa na Msajili hiyo awali Julai 17 mwaka huu alidai usajili huo ungefanyika baada ya kumaliza shughuli ya uhakiki wa vyama vya siasa uliaonza Julai 20 pamoja na kumaliza kazi hiyo aliendelea kuwa kimya na kuwaacha walioomba usajili wakilalamika.
Hata hivyo sababu hiyo inatupiliwa mbali na waanzilishi wa chama kipya kinacholalama kwa muda mrefu kupata usajili huo cha Independent Peoples Party (IPP), Andrew Bomani anayedai ofisi hiyo imekuwa na siasa na inakiuka sheria na katiba ya nchi.
“Kuna vyama vingi vimeomba usajili sheria inamtaka kuvitangaza kwenye gazeti la serikali kwa lugha mbili Kiswahili na Kiingereza na kutoa fursa watu kutoa pingamizi kwa wenye mashaka lakini hajafanya hivyo hatutendei haki,”amesema.
Akizunguma na Mwananchi leo, Jaji Mutungi amesema suala la kusajili vyama wasilichukulie kawaida huku akieleza kwa sasa mwingiliano wa watu nchini ni mkubwa na wanatumia fursa hiyo kujipenyeza kwenye vyama wakagombee vyeo.
“Suala la usajili wa vyama tusilichukulie kawaida, sasa tumeingiliana na watu wengi na njia kubwa wanayotumia ni kupitia vyama, hakuna kitu kina kera mwakani mnapata mgombea urais kumbe si Mtanzania kwa sababu njia pekee ya kugombea ni kupitia vyama,”amesema.
“Haya mambo haya siyo kila siku nikisimama nitaongea mbele ya umma lakini lazima mjue tuko makini, hii hatua ya watu kuanza kulazimisha. Tunaanza kuiwekea mashaka kwanini,”amesema.
Jaji Mutungi amesema historia inaonesha karibia kila uchaguzi mkuu kunaibuka vyama hivyo katika kuongeza utendaji na ufanisi wa shughuli hiyo ofisi hiyo haitaki kuweka kigezo cha uchaguzi tu isipokuwa wanahitaji kuona na hatua zingine zilizopo zifuatwe.
“Zamani ilikuwa watu wakileta fomu baada ya wiki mbili mnajiridhisha mnaamini imepitia kwenye kata yake lakini sikuhizi kuna mihuri ya ajabu ajabu kwahiyo sisi tuko makini kufuatilia,”amesema Mutungi.
Jaji Mutungi amesema katika mlolongo wa kutoa usajili wa muda hauishii kwenye ofisi hiyo pekee bali kuna taasisi zingine zinahusika.
“Kwahiyo kuchelewa kwa mchakato ni kwa sababu tuko makini kufuatilia uzalendo zaidi, mbona kuna Watanzania wengi tu wanaomba na wanatamani kuhama hata kwenye vyama vilivyopo kwenda kingine,”amesema.
“Kuna Watanzania wengine hawana passport lakini kuna raia wengine wa nje wanapasprt tuko makini kufuatilia na hatuna haja ya kumuonea mtu,”amesema.
“Uchaguzi ukiisha vuguvugu la vyama vya siasa linaisha kwanini kama wako makini na wanataka kucheza kwenye ulingo wa siasa huwezi kuunda chama leo na kwenda kugombea kesho hapo tunatilia shaka,” amesema.
Amesema huko nyuma kulikuwa na baadhi ya vyama viliomba usajili na vilikuwa na moto huo huo baada ya uchaguzi kupita waliingia mitini huku akieleza wasiipelekeshe ofisi hiyo inafanya kazi kwa kuzingatia taratibu.