Kesi ya Sabaya; Mawakili wachuana Vikali kwa saa tano

Kesi ya Sabaya; Mawakili wachuana Vikali kwa saa tano


Mabishano makali ya kisheria yameibuka mahakamani wakati Rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili ilipokuwa inasikilizwa mbele ya Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa.


Katika rufaa hiyo Jamhuri inapinga hukumu ya Mei 8, 2022 iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, iliyomuachia huru Sabaya na wenzake Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, baada ya mahakama hiyo kubaini kulikuwa na upungufu katika mwenendo wa kesi hiyo ikiwepo kutofautiana kwa ushahidi.


Rufaa hiyo namba 231/2022 itasikilizwa na jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Jacobs Mwambegele, Ignas Kitusi na Leila Mgonya.


Leo Novemba 1 wakati wa kuwasilisha rufaa hiyo, kulikuwa na mabishano yaliyomudu kwa zaidi ya saa tano kuanzia saa 5:08 asubuhi hadi saa 10; 40 jioni, ambapo walianza kuwasilisha hoja mawakili wa waleta rufaa kabla wajibu rufani hawajajibu.


Wakati mawakili wa mleta rufaa wakisema kwenye kesi ya msingi walithibitisha mshitaka yote bila kuacha shaka, upande wa wajibu rufaa walidai kuwa walishindwa kueleza hata eneo lilipo duka linalodaiwa kuwa mtaa wa bondeni, huku baadhi ya mashahidi wakidai duka hilo lipo Soko Kuu.


Katika kesi hiyo, mleta rufaa (DPP), amewakilishwa na jopo la mawakili wanne wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Chivanenda Luwongo, ambaye aliomna kufanya marekebisho ya hoja za rufaa kutoka saba hadi kufikia tatu baada ya kuunganisha sababu zingine na nyingine wakiondoa.


Akiwasilisha sababu hizo mahakani hapo, Wakili huyo ametaja sababu ya kwanza kuwa ni kuwa Mahakama ya Rufaa ya kwanza ilikosea kwa kusema kesi yao haina mashiko kwa sababu shahidi namba mbili hakuulizwa maswali na wajibu rufaa namba mbili na tatu na kufuta ushahidi wao wote na akawaachia huru.


Sababu nyingine ni mahakama hiyo kusema usikilizwaji wa awali wa kesi ulikosewa kwa sababu wajibu rufaa wawili (Nyegu na Mbura) hawakusomewa baadhi9 ya vitu wakati waliandika kwa maandishi kuwa wametimiza.


Ametaja sababu ya tatu kuwa ni Jamhuri haikuweza kuthibitisha kesi yao pasipo kuacha shaka, jambo ambalo amesema kesi hiyo ilitibitishwa pasipo kuacha shaka yoyote ambapo upande huo wa jamhuri walirejea ushahidi na vielelezo mbalimbali vilivyowasilishwa kwenye kesi ya msingi.


Aidha wakili huyo ameeleza mahakama kuwa ushahidi wa shahidi wa pili wa Jamhuri siyo ushahidi pekee uliowatia hatiani wajibu rufani hao na kuwa ushahidi wa mashahidi wengine na vielelezo viliwatia hatiani washitakiwa hao.


Hata hivyo, Wakili wa wajibu rufaa Mosses Mahuna, akijibu hoja hizo alirejea ushahidi uliotolewa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha akieleza ni msimamo wao kuwa hukumu ya rufaa ya kwanza ilikuwa sahihi na haikuwa na mapungufu yoyote.


Mahuna ameendelea kusisitiza msimamo wa kuwa utaratibu wa hoja za awali haukufuatwa kama ambavyo mahakama ya kwanza ya rufaa imeona na inatokana na upande wa jamhuri kushindwa kufanyia marekebisho hati ya mashitaka huku akinukuu mashauri mbalimbali.


Ameeleza kuwa ni uelewa wao kwamba haki yakusikilizwa ni moja ya haki ya msingi na kitendo cha mjibu rufaa wa pili na tatu kutopewa nafasi ya kumuuliza maswali ya dodoso kiliwanyima haki ya kusikilizwa na kuwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haisemi kiwango cha haki ya kusikilizwa.


"Kusema ushahidi wa shahidi wa pili wa Jamhuri haukutaka kuwatia hatiani, wakati huo ndiyo ushahidi pekee uliozungumzia wizi wa EFD mashine, watu kupigwa, wizi wa Sh2.689 milioni na ndiye alisema amemtambua mjibu rufaa wa pili nje ya duka (tukio lilipofanyika).


"Panapokuwa na utofauti kati ya hati ta mashataka na ushahidi njia pekee ni kubadili hati ya mashitaka na Jaji wa mahakama ile nyingine aliona kulikuwa na utofauti mkubwa kati ya hati ya mashitaka na ushahidi.


“Hati ya mashitaka inasema duka liko Bondeni, mashahidi wanasema liko SokoKuu, kielelezo cha 8 cha Jamhuri kinasema duka lipo Nyamwezi Street, leseni ya biashara inasema duka liko Bondeni street," amesema.


Umati wa watu ulifurika mahakamani hapo kufuatilia shauri hilo.


Mwenyekiti wa jopo hilo la Majaji, Jaji Mwambegele alieleza kuwa baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili watatafakari na kupitia hoja hizo na uamuzi utatolewa ambapo Msajili wa mahakama hiyo ambaye ndiye atausoma atatangaza tarehe ya uamuzi huo.


Hukumu anayoipinga DPP ilitolewa Mei 6, 2022 na Jaji Sedekia Kisanya wa mahakama Kuu Kanda ya Musoma ambaye alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuona kulikuwa na mkanganyiko kwenye mwenendo wa usikilizwaji wa shauri kwenye mahakama ya haki mkazi Arusha.


Alieleza kuwa kulikuwa na kutofautiana kwa mashahidi na kuufanya ushahidi kuwa batili na Mrufani namba mbili Nyegu na tatu Mbura hawakupewa haki ya kumhoji Shahidi namba mbili wa Jamhuri hivyo kunawanyima haki yao msingi.


Awali Oktoba 15, 2021 Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo, aliwahukumu Sabaya na wenzake wawili kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.


Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Amworo alisema ameridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka dhidi ya Sabaya na wenzake ambapo katika kesi hiyo Jamhuri ilikuwa na mashahidi 11 na vielelezo vinane.


Sabaya alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 4, mwaka 2021 baada ya kukamatwa Meo 27 wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad