KIMENUKA: Polisi wazagaa mitaani Mbeya, RC asema hajui sababu
Hofu na wasiwasi vimetanda kwa wananchi jijini Mbeya kufuatia askari polisi kuzagaa kwa makundi maeneo mbalimbali tofauti na siku nyingine.
Hata hivyo hakuna mamlaka yoyote iliyoeleza zaidi sababu za maaskari hao kutanda katika maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye shughuli za wananchi.
Mwananchi ilipita maeneo mbalimbali ikiwamo mitaa ya Kadege, Mahakama Kuu na kituo cha daladala cha Kabwe na kushuhuhudia askari wakiwa katika makundi wakiwa na vifaa vyao vya kazi.
Baadhi ya wananchi wamesema bado hawajaelewa lengo la askari hao kusambaa katika maeneo mbalimbali huku wengine wakihusisha na maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanywa na wanaojiita wanaharakati.
"Binafsi sijajua sababu zao kwa sababu hatujazoea labda kuwepo na jambo lolote, huenda wamejiandaa kuzuia maandamano tuliyosikia ila sina uhakika," amesema mwananchi huyo aliyekutwa stendi ya Kabwe akiomba kutotajwa majina.
Hivi karibuni mwanasheria wa kujitegemea Boniface Mwabukusi aliliambia gazeti hili kuwa wanakusudia kufanya maandamano leo Novemba 9, japokuwa Jeshi la Polisi lilipinga ombi hilo.
"Hata kama tumekosa kibali lakini sheria iko wazi kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana, hivyo msimamo wetu uko pale pale kufanya maandamano hayo ya amani kupinga kile tunachokiamini," amesema Mwabukusi.
Alipotafutwa mwanasheria na mwanaharakati huyo kuelezea msimamo wao, simu yake haikupatikana hewani.
Hata hivyo, maandamano hayo hayakuweza kufanyika wala kuwapo dalili yoyote kama ilivyokuwa imepangwa kuanzia Mtaa wa Kadege karibu na zilipo ofisi cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) .
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamini Kuzaga simu yake haikupokelewa, huku Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera akieleza kuwa hana taarifa zozote za kuwapo askari katika maeneo hayo.
"Kuna askari? Mimi sijaenda sehemu yoyote na sijui kama kuna hicho kitu, ngoja nifuatilie nione nitakupigia tena," amesema Homera.