Kocha Matola Awatuliza Mashabiki, Wanachama Simba SC

 

Kocha Matola Awatuliza Mashabiki, Wanachama Simba SC

Kaimu Kocha Msaidizi wa Simba SC, Seleman Matola, amewatuliza na kuwaomba Wanachama na Mashabiki wa timu hiyo, kurejesha ushirikiano na kuendelea kuwapa sapoti na kuachana na matokeo yote waliyopata katika michezo ya nyuma.

Matola ambaye amerejeshwa katika Benchi la Ufundi baada ya kuondoka kwa Kocha Robertinho na msaidizi wake Salami, amesema hakuna Mwanasimba ambaye hakuumia na matokeo ya kufungwa 5-1 na Young Africans.

Ameongeza kuwa hayo ni matokeo ya mpira ambayo yanaweza kutokea wakati wowote, aliwaomba wapenzi wa klabu hiyo, kusahau yaliyopita na kujipanga upya.

Matola amesema ameongea na wachezaji na wamemhakikishia katika michezo ijayo watajitahidi kupata matokeo mazuri.

“Kilichotokea kimetokea, tugange yajayo. Huu ni mpira na matokeo mabaya huwa yanatokea, kila mtu ameumia lakini kama ilivyo mikakati yetu ya ‘Nguvu Moja’, basi tuendelee kushikamana sababu tunayo nafasi ya kutwaa ubingwa.

“Ninawaomba mashabiki wetu waendelee kuipa sapoti timu, ninaamini tukishirikiana tutafikia malengo yetu, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu,” amesema Matola.

Amesema kwa sasa wameanza maandalizi ya kujiandaa mchezo wa kwanza wa Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika  dhidi na Asec Memosas ya Ivory Coast, mchezo utakaochezwa Novemba 25, mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Amesema wanajua wapinzani wao ni wazuri, wanajiandaa vyema kuhakikisha wanapata ushindi katika uwanja wa nyumbani na kuanza vyema kampeni za kutinga hatua ya Robo Fainali ya mashindano hayo.


“Tunakutana na mpizani mgumu na mwenye kikosi bora, tunaamini tutafanya vizuri, maandalizi tumeanza sasa kila mchezaji anatambua umuhimu wa kuanza vizuri mashindano hayo katika hatua ya makundi,” amesema.

Katika michuano hiyo, Simba SC imepangwa Kundi B pamoja na timu za Asec Memosas (Ivory Coast), Jwaneng Galaxy (Botswana) na Wydad Athletic Club (Morocco).

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad