Dar es Salaam. Aliyekuwa kocha wa Simba, Roberto Oliveira maarufuru kama Robertinho ameibua mpya baada ya kusema kati ya mastaa wapya tisa waliosajiliwa Simba wenye viwango vya ukubwa wa klabu hiyo ni wawili tu, Che Malone na Fabrice Ngoma.
Roberinho amesema hayo muda usiku wa kuamkia Ijumaa Novemba 10, dakika chache kabla ya kukwea pipa kuondoka kwenye ardhi ya Tanzania.
Maana yake ni kwamba, Luis Miquissone, Aubin Kramo na kipa Ayoub Lakred, David Kameta ‘Duchu’, Abdallah Khamis, Hussein Kazi, Hussein Abel na Shaaban Idd Chilunda ni wazuri lakini wa kawaida sana lakini hakuwa na namna ingawa amepambana na kupoteza mechi moja tu Msimbazi.
Kocha huyo ameng’olewa Simba kikubwa zaidi ikiwa ni baada ya timu hiyo kula kichapo cha mabao 5-1 dhidi ya Yanga, Jumapili iliyopita Kwenye Uwanja wa Mkapa. Robertinho aliondoka saa 5 usiku wa kuamkia jana, huku akisisitiza kwamba hana kinyongo na Simba lakini Che Malone na Ngoma ndiyo wachezaji wenye viwango bora katika usajili wa mwisho uliofanyika Simba. Kipigo dhidi ya Yanga ni cha kwanza kwake tangu ajiunge na timu hiyo Januari 3 mwaka huu na cha kwanza katika ligi kwa msimu huu pia cha kwanza tangu ilipofungwa na Azam Oktoba 27 mwaka jana.
Akizungumza na Mwananchi Digital, kocha huyo aliyeiongoza Simba kucheza mechi 19 za ligi, alisema katika usajili mpya ambao timu hiyo iliufanya msimu huu ni Ngoma na Che Malone ndio wachezaji wenye viwango na waliosalia ni papatu papatu tu!
Nyota hao wameungana na wakali wengine waliokuwepo msimu uliopita ambao Robertinho aliwakuta na kumaliza nao katika nafasi ya pili ya Ligi Kuu Bara nyuma ya Yanga, huku ikitoka kapa kwa kukosa tena mataji matatu iliyokuwa imeyapoteza kwa watani wao, likiwa Kombe la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii.
Msimu huu kocha huyo alirejesha Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga kwa penalti kwenye fainali iliyopigwa Tanga na juzi kabla ya kukwea pipa kurudi kwao, alisema Simba kwa sasa inabebwa na nyota hao wawili kwa wale waliosajiliwa msimu huu wanaoungana na wale waliowakuta kikosini.
Robertinho alisema bado timu hiyo inatakiwa kujengwa zaidi kufikia kwenye ubora ambao mashabiki wanautaka, kwa vile ina wachezaji wachache wenye viwango na waliosalia wanahitaji muda zaidi ya kujijenga kiasi hata mzunguko wa kubadilisha wachezaji ilikuwa ngumu kwake ingawa hakutaka kulalamika mbele ya mashabiki.
Beki Che Malone aliyesajiliwa kuwa Cotton Sport ya Cameroon amecheza mechi nane za ligi akitumikia dakika 720 akifuatiwa na Ngoma aliyetumika mechi zote nane kwa dakika 701. Robertinho alisema anatamani mashabiki wa Simba waelezwe ukweli halisi kwamba kikosi chao kina safari kwenda kwenye ubora stahiki, kuliko wanachoaminishwa kwa sasa kwamba tatizo ni kocha tu.
“Mashabiki wa Simba ni rafiki zangu watabaki kwenye moyo wangu wakati wote nitawakumbuka kila nilipokuwa nakutana nao viwanjani hata nikiwa matembezini walinipenda na nawapenda sana” alisema Robertinho na kuongeza;
“Lakini ni lazima waambiwe ukweli kwamba Simba ina safari ndefu kwa sasa kwa aina ya usajili uliofanyika na hata kwa wachezaji waliobaki kikosini, waliosajiliwa msimu huu ni Che Malone na Ngoma ndio wachezaji wenye ubora na viwango bora, wengine wanahitaji muda zaidi kuimarika.”
Alisema anaondoka Simba akiwa anajivunia rekodi nzuri aliyoiweka japo kipigo cha Yanga kimemtibulia, lakini anasisitiza amefurahia kuifundisha timu hiyo kongwe nchini na Afrika Mashariki.
“Safari yetu imeisha baada ya kupoteza mchezo mmoja tu, lakini nafurahi kuwaacha sehemu nzuri wakiwa juu ya msimamo na nimewapa heshima ya kuwa na taji, wanatakiwa kujua ukweli kwamba Simba ina timu nzuri lakini bado inahitaji kujengwa zaidi.
“Hakuna njia ya mkato kwenye kutafuta mafanikio kupata timu bora huwezi kuijenga kwa kutumia dirisha moja la usajili, ukiangalia safari ni hao wawili walioingia kikosi cha kwanza, waliosalia wanajitafuta. Jambo zuri Simba itajivunia tulibakiza wachezaji waliokuwa msingi wa timu ambao walipounganika na wengine tukajaribu kuwa na timu yenye upinzani.”
Robertinho alisema kwa sasa anarudi kwao Brazil kupumzika kwa muda na familia yake kabla ya kutafuta akili mpya ya maisha yake, huku akiweka bayana kwamba licha ya Simba kupoteza mechi moja bado ina nafasi ya kushindania ubingwa, kwa vile kuna mechi nyingi mbele kabla ya msimu kumalizika.
Simba kwa sasa ipo chini ya kocha wa makipa, Daniel Cadena akisaidiwa na Seleman Matola wakati mabosi wa klabu hiyo wakiendeleza na mchakato wa kupata kocha mkuu mpya wa kuziba nafasi ya Robertinho.
MTUNISIA ASEPA..
MSAIDIZI wa Robertinho, Ouanane Sallemi naye amepewa mkono wa kwaheri na juzi usiku alikuwa sambamba na bosi wake kurejea nchini kwao.
Kocha huyo Mtunisia alijiunga na Simba Januari 19 kwa mkataba wa miaka miwili, lakini kama ilivyokuwa kwa Robertinho na kocha wa viungo Corneille Hategekimana naye amefyekwa kutokana na kuipigo cha mabao 5-1 ilichopewa na Simba kwenye Kariakoo Derby.
Sallemi juzi saa 4:50 usiku akiwa na Robertinho aliondoka nchini kurudi kwao.
Robertihno na Sallemi aliwasili uwanjani hapo wakiwa na mabegi mawili tu, moja alilobeba Robertihno (saizi ya kati) na lingine la Sallemi lililokuwa kubwa kiasi.
Mwanaspoti ilikuwa uwanja wa ndege usiku huo huku makocha hao wakigoma kuweka bayana makubaliano ya fidia za kuvunjiwa mkataba alioingia na mabosi wa Simba.