Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amefichua siri iliyomvuta Kocha Mkuu wa klabu hiyo kwa sasa Abdelhak Benchikha ambaye tayari ameshawasili jijini Dar es salaam.
Kocha huyo anayetamba kwa kutwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga Young Africans msimu uliopita na CAF Super Cup kwa kuisasambua Al Ahly, amewasili nchini usiku wa kuamkia leo akiwa sambamba na wasaidizi wake Farid Zemiti (Kocha Msaidizi) na Kamal Boudjenane (kocha wa viungo).
Ahmed ally amefichua siri hiyo zikisalia saa kadhaa kabla ya kocha huyo kutambulishwa kwa Mashabiki na Wanachama wa Simba SC katika Mkutano na Maalum wa waandishi wa Habari utakaofanyika leo Jumanne (Novemba 28) jijini Dar es salaam.
Ahmed ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuainisha siri hiyo, huku akiwataja viongozi wa Simba SC kuwa chanzo cha ushawishi ambao ulifanikisha safari ya Benchikha kutoka Algeria hadi Tanzania.
Ahmed Ally ameandika: Kilichomvutia Mwalimu Benchika kujiunga na Simba ni mipango endelevu ya klabu yetu
Benchikha anataka kufanya kazi kwenye taasisi yenye maono mapana na yenye malengo makubwa
Benchikha ameangalia maendeleo yetu ndani ya kipindi cha miaka 6 na kujiridhisha kuwa Simba ni sehemu sahihi kwake
Imagine miaka 6 nyuma tulikua gizani lakini sasa SISI NI KLABU YA 8 KWA UBORA CAF kwa mujibu wa Takwimu rasmi za CAF sio takwimu za mashirika kilimo
Kama ndani ya miaka 6 tumeweza kufika nafasi ya 8 kwa ubora maana ake ndani ya miaka michache ijayo tutakua mbali zaidi, hiki ndicho kimemvutia Benchikha
Amevutiwa na project yetu na amejiridhisha kuwa viongozi wapo Serious na hatimae amekubali kufanya kazi na sisi
Najua wengi mtakimbilia kusema mbona mmepoteza mechi tatu hayo ni matokeo hayatibui malengo na maendeleo yetu
Winning & Success (Ushindi na Mafanikio)