Latra yatangaza nauli mpya za daladala, mabasi



Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), leo Jumatatu Novemba 27, 2023 imetangaza nauli mpya za mabasi ya mjini (daladala) na za masafa marefu ambazo zimepanda kwa viwango tofauti kulingana na umbali na aina ya barabara.

Nauli mpya zimetangazwa na Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo jijini Arusha huku sababu ikitajwa kuwa ni ongezeko la gharama za uendeshaji ikiwamo kupaa kwa bei za mafuta (petroli na dizeli).

Suluo amesema daladala zenye ruti isiyozidi kilomita 10 itapanda kutoka Sh500 hadi Sh600, ruti ya kilomita 11 hadi 15 nauli itaongezeka kutoka Sh550 hadi Sh700 na ruti ya kilomita 16 hadi 20 nauli itaongezeka kutoka Sh600 hadi Sh800.

“Daladala zilizokuwa na ruti ya umbali wa kilomita 21 ha 25 nauli itapanda kutoka Sh700 hadi Sh900, zile zenye ruti ya kilomita 26 hadi 30 nauli itapaa kutoka Sh850 hadi Sh1,100,”amesema Suluo.

Taarifa iliyotolewa na Latra pia imesema, kwa daladala ambazo zilikuwa zinatoza Sh1,000 (umbali wa kilomita 31 hadi 35) bei itapanda hadi Sh1,300 na zile zenye ruti ambazo umbali wake ni kati ya kilomita 36 hadi 40, bei ya nauli itapanda kutoka Sh1,100 hadi Sh1,400.

Wakati nauli zikipaa kwa upande wa daladala kwa wastani wa asilimia 10, pia mabasi ya masafa marefu nauli itapaa kulingana na daraja la basi na aina ya barabara inayotumika.

“Mabasi ya daraja la kawaida katika barabara ya lami kila kilomita moja itatoza Sh48.47 kutoka Sh41.29 kama ilivyokuwa awali na kwa barabara ya vumbi daraja hilo litatoza nauli ya Sh53.32 kwa kilomita kutoka Sh51.61,”imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Pia, nauli itapanda kwa mabasi ya daraja la kati (luxury na semi-luxury) kwa barabara ya lami nauli itapanda kutoka Sh56.88 kwa kilomita hadi Sh67.84.

Aidha, Latra imesema kuwa viwango hivyo vipya vya nauli vinajumuisha tozo ya asilimia 0.5 inayotozwa na mamlaka hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad