Nyota wa Simba ambao hawapo timu za taifa wanaendelea kujifua kambini Mo Simba Arena, Bunju Dar es Salaam kujiandaa na mechi ya kwanza ya Kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Ases Mimosas ya Ivory Coast, huku mabosi wao jana wakiitana na kujifungia jijini humo kwa saa kadhaa.
Simba itakuwa wenyeji wa Asec Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku mabosi wakiendelea kukuna vichwa kusaka kocha mpya kabla ya mchezo huo na jana Jumamosi jioni waliamua kujifungia ili kujadili kwa kina kupata muafaka wa kocha gani wamlete kushika mikoba iliyoachwa na Roberto Oliveira ‘Robertinho’ waliyemtimua.
Robertinho, raia wa Brazil alitimuliwa sambamba na wasaidizi wake Cornelly Hategikimana na Oumane Sallemi baada ya kichapo cha mabao 5-1 kutoka kwa watani zao, Yanga mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Novemba 5 Kwa Mkapa.
Kwa sasa Simba inanolewa na kaimu kocha mkuu, Daniel Cadena aliyekuwa akiwanoa makipa chini ya Robertinho akisaidiana na nyota wa zamani wa timu hiyo, Seleman Matola na tayari kulikuwa na majina matatu ya mwisho mezani mwa vigogo akiwamo Sven Vandenbroeck, Nasreddine Nabi na Abdelhak Benchikha. Sven na Nabi wameshapigwa panga kutokana na sababu mbalimbali, huku Benchikha naye akiwa kwenye hatihati kutokana na dau analotaka kuwayumbisha mabosi wa klabu hiyo.
Hata hivyo hatima ya mwisho juu ya kocha huyo wa zamani wa USM Alger ilikuwa ikijadiliwa jana na kama wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wataamua kumtema, basi kuna uwezekano Daniel Cadena akaachiwa timu hadi mchakato mpya utakapofanyika.
“Leo (jana) jioni tutakutana tena na kujadiliana kwa kina kujua hatima ya kocha mpya. Pia kuna mengine yatakayojadiliwa kwa ajili ya mechi ya Asec Mimosas,” alisema mmoja wa vigogo wa Simba alipoulizwa juu ya kikao hicho