Madeleka Ahojiwa Polisi Akidaiwa Mtoro Kazi ya Upolisi




Arusha. Wakili maarufu nchini, Peter Madeleka leo amehojiwa kituo kikuu cha Polisi jijini Arusha, kwa saa moja akidaiwa amekuwa mtoro kazini Jeshi la Polisi.

Kabla ya kuwa wakili, Madeleka alikuwa na Mkaguzi wa Polisi kitengo cha upelelezi Makao makuu ya Polisi Dar es Salaam na baadaye alihamishiwa Zanzibar, kabla ya kuacha kazi mwaka 2016.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa Arusha, Salvas Makweli alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa wakili huyo, alisema hana taarifa.

"Leo siku nzima nipo nje ya ofisi kushughulikia suala la mafuriko hivyo sina hizo taarifa za Madeleka kuhojiwa," amesema.


Akizungumza na Mwananchi Leo Novemba 13, 2023 Wakili Madeleka amesema ameshangazwa kuitwa polisi na kuhojiwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ASP) Mdoe kwa tuhuma kuwa yeye ni mtoro kazini.

Madeleka amesema, yeye aliacha kazi ya polisi tangu mwaka 2016 na alifuata taratibu zote za kuacha kazi kama mtumishi wa umma.

"Tangu mwaka 2016 kwa kuwa niliacha kazi, sijalipwa mshahara lakini pia mwaka 2019 hadi 2021 nilikuwa Magereza nimefungwa sasa kama nilikuwa polisi mtoro ilikuwaje wanikamate na kunifunga," amesema.


Amesema hata baada ya kutoka Magereza alikamatwa tena Julai mwaka huu baada ya kurejeshwa shitaka lake Mahakamani la kupinga kukiri makosa na alikaa Magereza hadi Septemba mwaka huu.

"Sasa kama wanasema mimi ni polisi mbona muda wote huo nipo barabarani hawajawahi kunikamata kwa utoro kazini," amesema.

Amesema kwa mujibu wa sheria za kazi, mfanyakazi wa umma akiwa hayupo kituo cha kazi bila taarifa siku 14 tu anapaswa kufukuzwa.

"Nimewambia ASP Mdoe kama wanasema Mimi ni polisi mtoro kazini basi waniachishe kazi, lakini nimewaeleza mimi sio polisi watafute nyaraka zangu za kuacha kazi," amesema.


Amesema baada ya kutoa maelezo hayo ameachiwa bila masharti na anaendelea na majukumu yake.

Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad