. CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeagiza pikipiki zote zilizokamatwa kwenye kituo cha polisi cha Sirari kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya ziachiwe haraka.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi, Paul Makonda alitoa agizo hilo wakati akizungumza na maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Bibi uliopo Wilaya ya Tarime mkoani Mara.
"Chama kinaagiza vijana wote wa bodaboda wa Sirari kesho warudishiwe bodaboda zao na kama kuna mali zao zilizokamatwa wahusika watozwe kodi warudishiwe mali zao, lakini waendelee kufuata sheria," amesema Makonda.
Amesema CCM inamuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda ndani ya siku tatu awe ameshawasilisha mpango mkakati wa namna atakavyotatua migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Mara.
“Chama hakitaki kusikia wala kuona migogoro inaendelea kuwepo katika Mkoa wa Mara," amesema Makonda.
Mtanda ameagiza wakuu wote wa wilaya za mkoa huo kuanzia Novemba 20, mwaka huu wakae na maofisa na wataalamu wa ardhi ili kutatua changamoto hiyo.