Simba SC, juzi Jumapili ilikubali kipigo cha mabao 5-1 dhidi ya Yanga, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Yanga ilifunga mabao yake kupitia Kennedy Musonda, Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili. Simba mfungaji wao ni Kibu Denis.
Baada ya mchezo huo, wachezaji wa Simba wametupiwa lawama kutokana na kipigo hicho. Hapa Spoti Xtra tunakuchambulia mambo matatu yaliyofanya Simba kupokea kipigo hicho kikali kutoka kwa watani zao wa jadi, Yanga.
KIWANGO CHA MANULA
Haikuwa siku nzuri kwa kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula ambaye ndiye alikuwa amerejea uwanjani baada ya kukaa nje kwa takribani siku 212 akiuguza majeraha ya nyonga.
Kabla ya juzi, mara ya mwisho Manula kuidakia Simba ilikuwa Aprili 7, 2023 katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar, Simba ikashinda 5-1.
Kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi saba bila ya kucheza mechi za kimashindano, anakuja kuonekana mbele ya watani wao wa jadi, Yanga.
Katika mchezo wa juzi, Manula alionekana kutokuwa tayari kwa kiasi kikubwa na kufanya kuruhusu mabao hayo ambayo baadhi mpira ulimpita bila ya kufanya lolote.
Bao la kwanza alilofungwa na Musonda, hakuruka zaidi ya kuusindikiza mpira kwenye nyavu, huku pia hakuwa akizungumza sana na walinzi wake katika kuwapanga kuzuia mashambulizi.
SAFU YA ULINZI SIMBA
Mabeki wa kati, Che Malone Fondoh na Henock Inonga, na wale wa pembeni, Mohamed Hussein na Shomari Kapombe, hawakuwa wakikaba kwa nidhamu.
Mara kadhaa walikuwa wakiwaacha wachezaji wa kufika eneo lao la hatari na kuwasumbua. Walikuwa wakikaba kwa macho, huku wakiacha mianya kwa wapinzani.
Mfano bao la kwanza, Musonda aliruka kichwa katikati ya walinzi wawili wa Simba, Kapombe na Che Malone. Pia bao la pili, Maxi anapita katikati ya Kapombe na Che Malone, anakwenda kufunga.
Bao la Aziz Ki, Yanga walitumia udhaifu wa Simba waliokwenda kushambulia na kuacha lango lango lao. Mohamed Hussein, alishindwa kurudi haraka eneo lake la kushoto, Clement Mzize akautumia mwanya huo kutengeneza nafasi ya bao kama ilivyokuwa bao la nne lililofungwa na Maxi ambaye aliachwa peke yake na Kapombe.
UBORA WA YANGA
Yanga walikuwa na siku bora sana katika mchezo wa juzi, hali iliyofanya Simba waonekana dhaifu muda mwingi wa mchezo hasa kipindi cha pili.
Ukiangalia eneo la kiungo, Yanga walitawala kwa kiasi kikubwa, Pacome, Khalid Aucho na Mudathir Yahya, walikuwa wanafanya watakavyo dhidi ya kina Fabrice Ngoma na Sadio Kanoute.