Mashabiki kindaki ndaki wa Klabu ya Simba, Pasi Milioni na Kisugu wameutaka uongozi wa timu hiyo kufanya maamuzi magumu kwa kuwafukuza wachezaji wasiojituma ambao wamekuwa wakiihujumu timu.
Hii ni baada ya timu hiyo kushindwa kupata matokeo mazuri kwenye mechi mbili ikiwa ni kipigo cha bao 5-1 kutoka kwa Yanga na sare ya bao 1-1 kutoka kwa Namungo FC.
“Timu yetu ya Simba inavyocheza ninaona kiwango kimeshuka, ninawashangaa sana watu wanapoanza kuwashambulia viongozi wa klabu wakati ukiangalia unaona viongozi wanalipa kwa wakati, bonsai kwa wakati na ndio timu pekee inayolipa mshahara mkubwa kuliko timu yoyote Afrika Mashariki na Kati, sio Tanzania tu.
“Tuna mchezaji tuna mlipa Tsh milioni 35, hakuna timu nyingine Tanzania. Ifike wakati wachezaji wetu wabadilike, wajitume, wapambane, usipopambana huwezi kumfunga mtu. Wachezaji waone aibu, watuhurumie na sisi ambao tunaacha familia zetu kwenda mikoani mpaka nje ya nchi kuwasapoti, tumekwenda Zambia kilomita 3,800 kwenda na kurudi kwa ajili ya kutafuta furaha lakini kwa nini hawataki kujituma?
“Lazima tujue kila mmoja ana majukumu yake kwenye soka, uongozi hauingii uwanjani kucheza dakika 90, viongozi wa Simba wanatekeleza majukumu yao kwa kusajili, wanawapeleka wachezaji kambi, wanalipa kila kitu, lakini ifike wakati tuseme ukweli kwamba morali ya upambanaji ya wachezaji imeshuka.
“Simba iliyocheza na Al Ahly mabingwa namba moja Afrika sio Simba iliyocheza na Yanga wala Namungo. Mechi ya Ahly morali ilikuwa kubwa, wachezaji walikuwa wanapambana, lakini leo inacheza kama wachezaji wamekuja kufanya mazoezi, tumechoka. Simba ni kubwa kuliko mtu yeyote, wengi wamepita, kama wewe unaona hustahili kucheza Simba tupishe, sio kutupa maumivu kila siku.
“Kuna wachezaji wametengeneza mazingira ya kwamba watapoteza dakika 90 halafu lawama zitakwenda kwa mangungu wao wataendelea na maisha yao, ifike wakati viongozi wafanya maamuzi magumu. Tunahitaji kuona marekebisho makubwa kwenye dirisha dogo, wachezaji wanaonekana hawataki kuipambania Simba. Tunafungwaje, tunapotezaje?
“Hatuwezi kuwa na wachezaji wanakimbia kama wamekanyaga miiba, inasikitisha. Simba inafungwa, mchezaji anapiga selfie? Una raha gani wewe? Sisi tunaumia, inakera, inaumiza na inauma. Wachezaji hawajachoka, si ndio hawa hawa wamecheza na Ahly juzi? Mchezaji unafungwa bao 5 unacheka watu wanazimia?
“Unamlaumu kiongozi kwani ndiye alikaa golini au alicheza beki, au kiungo ama alikuwa mshambuliaji? Wasitake kuturudisha kama zamani, mechi kama hizi wachezaji walikuwa wakizingua wanachapwa bakora. Simba sio kuku wala Simba hanyatiwi.
“Wachezaji wanawachonganisha mashabiki na viongozi, watoke waseme mishahara hatulipwi. Ukivaa hii jezi kwa ajili ya Simba unatakiwa utoke jasho na damu, kama huwezi tupishe, timu ziko nyingi. Tumechoka, tunawaambia wachezaji wa Simba tumechoka.
“Tumecheza na Yanga kipindi cha kwanza wachezaji wamepambana, tukajua leo mechi ni yetu, kipindi cha pili sio Simba ile, ni jezi tu zimevaliwa. Watu zaidi ya nane wamekufa ile mechi, ndugu zao wamepata faida gani? Wanatufanya kutugombanisha na viongozi mara tunaitwa chawa mara kunguni, wachezaji hawatutendei haki.
“Viongozi wa Simba tuwaambie tu ukweli, wasiwahurumie hawa wachezaji, wawafyatue, ondoa kabisa. Dirisha dogo mbali sana, kesho tu waondoke. Wapo wachezaji wanaojituma uwanjani mpaka unawaonea huruma, wengiune wanatembea tu uwanjani,” wamesema mashabiki hao.