Mbunge wa Mbarali (CCM), Bahati Ndingo amewataka wataalam wanaobahatika kupata nafasi ya kumshauri Rais, waache uvivu wa kufikiri.
Mbunge huyo pia amemuomba Waziri wa Mpango Profesa kitila Mkumbo kusoma taarifa za mpango wa mataifa mengine kama Zambia, Kongo na Mexco ili ajifunze namna walivyosaidia wananchi wao kwenye maeneo kama Mbarali.
Ndingo ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Novemba 6, 2023 ikiwa mara yake ya kwanza tangu alipochaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo Oktoba 19, 2023 kufuatia kifo cha Francis Mtega, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, ambacho kilitokea Julai Mosi mwaka huu.
Ndingo amesema kitendo cha kuamua kuwaondoa wananchi wa Mbarali ili kupisha uhifadhi hakikubariki na kwamba hatakuwa tayari kuona hayo yakifanyika.
“Mnapanga kitu gani, mnafikiria kuwaondoa wananchi wa wilaya hiyo bila huruma, tatizo mnaopata nafasi ya kumshauri Rais, mnakuwa wavivu wa kufikiri, acheni hayo ili muweze kumsaidia Rais,” amesema Ndingo.