Mikataba ya Plea Bargaining moto, Bunge lacharuka




Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeitaka Serikali kuchunguza na kuwachukulia hatua wahusika wa dosari za Uendeshaji na Usimamizi wa Mikataba ya Maridhiano ya Kukiri Makosa (Plea Bargaining).

Mjadala wa taarifa za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2022 ulianza bungeni jana na utafanyika kwa siku tatu hadi kesho.

Taarifa za CAG ziliwasilishwa bungeni kwenye Bunge la Aprili na Spika Dk Tulia Ackson, aliyewaeleza wabunge mjadala wa taarifa hizo utafanyika kwenye Bunge hili la Novemba.

Akizungumza bungeni jana, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Japheti Hasunga alieleza maoni ya uchambuzi wa kamati yake kuhusu ‘Plea Bargaining’ wakitaka Serikali ichunguze kwa kina.


“Serikali ifanye uchunguzi wa kina na mahsusi katika suala hili kwa kuzingatia masharti ya Katiba na Sheria ili wahusika wachukuliwe hatua ipasavyo kwa dosari zilizojitokeza katika mchakato huu,” alisema Hasunga.

Maoni ya PAC yanakuja wakati kukiwa na mapendekezo ya CAG, Charles Kichere akipendekeza mamlaka ya uteuzi kumchunguza (bila kumtaja jina) Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ambaye kwa wakati huo alikuwa Biswalo Mganga, kwa sasa ni jaji.

“Napendekeza mamlaka za uteuzi za aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ziunde Tume huru ya kuchunguza uwezekano wa ukiukwaji wa maadili na matumizi mabaya ya ofisi ya umma katika mchakato wa makubaliano ya kukiri kosa,” alisema Kichere.


“Tume hiyo inapaswa kuchunguza madai ya kulazimishwa kwa washitakiwa na ukikwaji wa Kanuni za Mwenendo wa Mashtaka ya Jinai (makubaliano ya kukiri kosa) za mwaka 2021 na kutoa mapendekezo ya uboreshaji wa upungufu wote uliobainika.”

Pia, Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizindua Tume ya Haki Jinai alionyesha kushangazwa na fedha hizo kugundulika nyingine ziko kwenye akaunti za benki nchini China na aliitaka tume hiyo kuchunguza suala hilo kwa kina.

Hasunga alisema kamati iliangalia hasara ya zaidi ya Sh7.8 bilioni katika kampuni ya mafuta ya Tanoil, kwamba inachangia upotevu wa mapato ya Serikali na hivyo kutofikiwa lengo la kuanzishwa kwa kampuni hiyo.

“CAG azingatie kupitia kwa kina utaratibu uliotumika kuanzisha kampuni hiyo na malengo yake, kupitia na kuchambua utaratibu na njia za kibiashara zinazotumiwa na Tanoil kufanya biashara ya mafuta na endapo zina tija na ufanisi,” alisema Hasunga.


Pia, alisema kamati yake imeshauri uchunguzi ufanyike kwa iliyokuwa menejimenti na uongozi wa Tanoil katika kusababisha hasara kwa kampuni, hasa kwa maamuzi waliyokuwa wanafanya kinyume na taratibu na miongozo.

Akichangia mjadala kwenye taarifa ya PAC, mbunge wa Busega (CCM), Simon Lusengekile alitaka kufanyika kwa ukaguzi wa kiuchunguzi kwa kampuni ya mafuta ya Tanoil ili wote waliohusika na hasara ya Sh7.8 bilioni wajulikane na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema hasara hiyo imetokana na uamuzi wa kupunguza bei ya mafuta uliotolewa na watendaji bila kuzingatia kanuni wala kuishirikisha bodi, wakurugenzi na waziri husika.

“Lakini wao wanajichukulia maamuzi, hawana kibali, wanajichukulia wenyewe, kupunguza bei haiwezekani. Wanatuzunguka wanakwenda kuuza na kuchukua cha juu. Naomba Waziri wa Nishati akaanze na hili, tukubaliane CAG akafanye ukaguzi wa kiuchunguzi kuona wale waliosababisha hasara ya Sh7.8 bilioni,” alisema Lusengekile.


Baadhi ya waliokumbwa na utaratibu wa kukiri kosa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), Harbinder Seth aliyetakiwa kulipa Sh26.9 bilioni baada ya kukutwa na hatia ya kujipatia Sh309 bilioni kwa njia ya udanganyifu.

 Wengine ni Deogratius Mwanyika aliyekuwa Rais wa mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu, ambaye pamoja na wenzake sita walitakiwa kukubali kulipa fidia ya Sh1.5 bilioni kila mmoja.

 Mbali na Mwanyika, pia Mkurugenzi wa Kampuni ya Mr Kuku Farmer Ltd, Tariq Machibya maarufu Mr Kuku ni mwathirika mwingine aliyetakiwa kulipa fidia ya zaidi ya Sh5.4 bilioni, Desemba 16, 2020 baada ya kukiri mashitaka ya kushiriki katika upatu na kupokea miamala ya fedha kutoka kwa umma.

Kamati ya LAAC

Mbali na PAC, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambayo ndiyo jicho la Bunge katika kushughulikia matatizo ya matumizi mabaya ya fedha za umma ilichambua maeneo kadhaa yenye changamoto ya matumizi mabaya ya fedha za umma yaliyobainishwa katika taarifa ya CAG, yakiwamo ya ununuzi uliofanywa na halmashauri wa Sh106 bilioni uliokiuka matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na kanuni zake.

Mwenyekiti wa LAAC, Halima Mdee akitoa maoni ya kamati yake bungeni alisema walichambua changamoto ya matumizi mabaya ya fedha za umma, kutokuwepo kwa ufanisi wa utendaji wa wakurugenzi, kukosekana kwa uthubutu wa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kushindwa kuzuia mianya ya upotevu wa mapato ya ndani, hali inayosababisha halmashauri nyingi kushindwa kufikia lengo la ukusanyaji wa mapato.


Alisema kutokana na upungufu uliobainika kwenye halmashauri nyingi nchini, kamati yake imependekeza Serikali iandae mikataba ya utendaji kazi na ukusanyaji wa mapato ya ndani itakayokuwa na vigezo kwa wakurugenzi wote.

“Aidha katika kila robo mwaka, kila Katibu Tawala Mkoa afanye tathimini iwapo wakurugenzi hao wamefikia malengo ya ukusanyaji wa mapato na kuwasilisha taarifa hiyo Ofisi ya Rais (Tamisemi) kwa hatua stahiki,” alisema Mdee.

“Serikali ihakikishe fedha zote zilizokusanywa kupitia mashine za kukusanya mapato (POS) Sh11.7 bilioni zinawasilishwa Benki kabla ya Aprili, 2024 na watendaji wote waliohusiwa wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema.

Kuhusu matumizi yasiyofaa ya fedha za umma, Mdee alisema maoni ya kamati ni kuitaka Serikali iwachukulie hatua za kinidhamu watumishi wote waliofanya malipo kwa fedha taslimu kwa kiasi kilichohojiwa cha Sh1.51 bilioni kinyume na mwongozo wa Uhasibu wa Halmashauri wa Mwaka 2021.

“Serikali ichukue hatua za kinidhamu na kisheria kwa watu wote waliofanya matumizi ya Sh11.78 bilioni bila nyaraka halali za matumizi hayo,” alisema.

Mdee alisema kamati imependekeza kutokana na halmashauri nyingi kubainika kukiuka Sheria ya Ununuzi wa Umma, Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ifanye ukaguzi wa kina katika maeneo yote yaliyobainishwa katika ripoti ya CAG.

Akichangia taarifa ya kamati ya LAAC kuhusu kasoro kwenye halmashauri, mbunge wa viti maalumu (CCM), Suma Fyandomo alisema halmashauri zina wakurugenzi ambao sio waaminifu na kuwa Serikali ilianzisha utaratibu wa ‘force account’ kwa nia njema, lakini kwa upande mwingine halmashauri nyingine zinafanya vibaya.

“Hizi fedha ni za walipa kodi masikini kabisa wa Taifa hili, utakuta mkurugenzi anakutwa na CAG majengo ambayo yamejengwa, ni mapya yanavyokaguliwa yana nyufa. Majengo milango inadondoka yenyewe kabla ya kuanza kutumika, lakini alikuwepo mkurugenzi kuyasimamia,” alisema.

Mbunge wa Mtoni (CCM), Abdulhafar Idrissa Juma akichangia mjadala huo aliitaka Serikali kuboresha hatua za kinidhamu zinazochukuliwa kwa watendaji wabadhirifu kabla ya kuwapeleka katika hatua za kisheria.

“Nikwambie yuko mkurugenzi ana kesi ya jinai kwa matendo aliyoyafanya katika halmashauri moja, sasa hivi ni mkurugenzi katika halmashauri nyingine anatoka na gari la Serikali anakwenda kuhudhuria kesi alilolifanya katika halmashauri fulani,” alisema.

Mbunge wa viti maalumu, Conchesta Rwamlaza aliwataka baadhi ya watendaji wa halmashauri nchini kuacha roho mbaya na badala yake kuwalipa wazabuni wanaowadai.

“Ukitaka kufa masikini nchi hii fanya kazi na halmashauri, utatembea kudai hadi visigino vikatike, na taarifa za chini zinasema kama hujatoa kitu chochote hulipwi,” alisema Rwamlaza.

Mbunge wa Lulindi (CCM), Issa Mchungahela alisema changamoto kubwa ya Taifa ni watu wake kukosa uzalendo, hivyo inawapa tabu kutathimini na kuangalia jinsi uzalendo unavyopatikana.

“Licha ya kuaminiwa na mheshimiwa Rais, wale walioteuliwa na watu mbalimbali bado kumekuwa na changamoto, hatutendei haki teuzi hizo wala hatutendei haki kuchaguliwa huko,” alisema Mchungahela.

Alisema kumekuwa na shida ya upotevu wa maadili katika taasisi mbalimbali na kuwa katika mahojiano ya taasisi nyingi amebaini maofisa masuhuli wengi hawatambui majukumu yao au kwa makusudi wameamua kutoyatekeleza.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad